Thursday, August 17, 2017
MBINU ZA KUKUA KIBIASHARA NA KIMAISHA
Mbinu za kupata mtaji wa biashara
Watu wengi wanatamani kumiliki biashara siku moja na huenda wana mipango mizuri juu ya bishara zao. Mipango hii inaweza ikawa vichwani tu au mingine katika maadishi lakini inapofika wakati wa utekelezaji wa mipango hii ukosefu wa mtaji wa biashara hiyo ni kipingamizi kwa wengi.
Lakini kuna jinsi kadhaa ambazo zinaweza kusaidia upatikanaji wa mitaji kwajili ya biashara.
Aina Za Mitaji
Kuna aina mbili ya mitaji kwaajili ya biashara au uwekezaji wa aina yoyote.
• Mtaji wa Mkopo
• Mtaji wa Mmiliki
Mtaji wa Mkopo unakuwezesha kukopa toka kwa taasisi za fedha au mtu binafsi wakiwemo ndugu ,jamaa na marafiki na kuhitajika kulipa katika kipindi maalumu ikiwa pamoja na riba au bila riba.
Aina hii ya mtaji inakuwezesha kufanya biashara lakini ni lazima uwe makini katika utunzaji wa fedha zako na uzalishaji wake kwani mwishowe utahitajika kurudisha fedha zote pamoja na riba pengine kila mwezi.
Mtaji wa Mmiliki ni mtaji toka kwa mtu au kampuni ambayo inahitaji kuwa na umiliki wa sehemu ya bishara. Hawa wanataka kupata faida kutokana na uwekezaji katika kampuni au biashara yako.
Kama uko tayari kutoa sehemu ya umiliki wa biashara yako basi mtaji wa aina hii utakusaidia kuanzisha au kuboresha bishara yako.
Changamoto Za Kupata Mitaji:
Kupata mtaji wa biashara ni changamoto kubwa kwa wajasiriamali kote duniani. Japo fedha za mikopo zinapatikana katika mabenki lakini bishara nyingi hazina miundo mizuri na mifumo ya fedha kuwezesha kupata mikopo. Benki zimekuwa na masharti magumu sana kiasi kwamba bishara nyingi haziangalii huko kama sehemu ya kupata mikopo.
Mikopo toka kwa ndugu na jamaa pia ina changamoto zake,si rahisi ndugu au rafiki akakuamini au akaamini kuwa biashara yako itafanikiwa,tunajua asilimia 90 za biashara zinazoanza zinakufa kila mwaka. Hili linawapa wasiwasi sana wakopeshaji.
Mambo Ya Kuangalia Kabla Ya Kupata Mtaji
Mtaji Toka Kwenye Mikopo:
Ili kupata mikopo kunahitajika dhamana kuwahakikishia wakopeshaji wako kuwa kama hutafanikiwa basi ni kwa jinsi gani fedha zao zitarudi.
Na utakutana na msharti mengi magumu,dhamana inaweza kuwa kama ifuatavyo:
• Nyumba
• Kiwanja
• Shamba
• Gari
• Mali za nyumbani au ofisini(biashara yenyewe)
• Ni lazima ujiulize mapema kama uko tayari kuweka mojawapo ya vitu hivi kuwa dhamana.
Kwa namna hii ni rahisi kupata mkopo na ni lazima urudishe deni vinginevyo utapoteza.
Huu ndio ujasiriamali wenyewe, uthubutu wa kufanya mambo ya hatari katika harakati za kufanikiwa katika biashara.
Mtaji Toka Kwa Wawekezaji:
Kama utaamua kuingiza wawekezaji wengine katika biashara yako basi pia nilazima ufikirie mapema kuwa kutakuwa na taarifa ambazo watahitaji kujua juu ya mwenendo wa biashara yako.
• Je unapata faida kwa sasa?
• Muelekeo ukoje,unapanda na bidhaa au huduma zinahitajika?
• Ni kwa namna ipi fedha zinzohitajika zitawekezwa ili kuboresha biashara na kuleta faida kwa haraka n.k
• Waekezaji nao wanaangalia hatari ya kupoteza fedha zao na pia muda wa kurudisha fedha wanazowekeza na faida itakayozalishwa.
Kama biashara yako haiwezi kuonyesha haya kabla,ni ngumu kupata wawekezaji katika bishara yako.
Mpango Bishara na utunzaji mzuri wa mahesabu ya biashara yako yatasaidia sana kutoa taarifa hizi na hivyo kukusaidia kupata wawekezaji
Taarifa Za Fedha Na Mpango Wa Bishara Ni Nyenzo Muhimu Kupata Mtaji Wa Biashara
Kama ni niashara mpya ,kutahitajika kuwa na mpango wa biahsara,andiko ambalo linaelezea jinsi ambavyo biashara yako itafanyika ,kiasi cha fedha kinachohitajika, bidhaa na huduma utakazo toa ,masoko,na wafanyakazi.
Andiko hili litasaidia kushwawishi wawekezaji na watoa mikopo.
Kama biashara yako iko tayari na unataka kuongezea mtaji, basi utahitaji kuwa na taarifa za hali ya fedha ya bishara yako, pia unaweza ukaandaa mpango wa biashara unaoelezea mwelekeo wa biashara katika miaka kadhaa mbele.
Wafanyabishara wengi wa kati na wa chini hawafanyi haya, ndio maana kunakuwa na ugumu kupata mitaji ya kuanzia au kukuza biashara.
Huenda ukahitaji msaada toka kwa wataalamu wa biashara na upate usaidizi wa kitaalamu,andaa fedha kidogo kwajili ya huduma hizi. Kuna makampuni mengi tu sasa hivi ambayo yanatoa huduma kwa wafanyabiashara kwa gharama ndogo.
Mbinu 5 Za Kupata Mtaji Wa Biashara:
Aina hizi zote za kupata mitaji zinaingia katika makundi mawili yaliyotajwa hapo awali aidha ni mkopo au uwekezaji
1. Mkopo Toka Benki Au Tasisi Za Mikopo
Benki zote hutoa mikopo kwaajili ya biashara ila taarifa za muhimu zinahitajika kuhusu mwenendo wa biashara kama tayari imeshaanza au Mpango wa biashara unaoelezea jinsi ambavyo biashara itaendeshwa na jinsi ambavyo deni litalipwa.
Benki huhitaji vitu vya thamani kwajili ya dhamana ya fedha watakazokupa kama mtaji.
Iwapo fedha hazitarudishwa kama ambavyo iliwekwa katika masharti ya mkopo basi mali hiyo itauzwa ili kufidia deni.
Hili limekuwa ni changamoto kwa wengi kupata mikopo toka benki. Hasa kwa biashara anbazo zinaanza na hazina uhakika wa kufanya vizuri na uwezo wake wa kurudisha deni.
Aina hii ya mikopo inaweza ikawasaidia wale ambao bishara zao zimeshasimama na wanafanya kwa faida. Pia kwa zile biashara ambazo mzunguko wa fedha ni mkubwa na hawatahitaji muda mrefu wa kulipa deni.
Benki mpya mara nyingi huwa na msharti rahisi kuliko benki kongwe.
Aina nyingine ya mikopo ambayo inafanana na ile ya benki ni toka katika taasisi za mikopo. Taasisi hizi zinatoa masharti nafuu kido kuliko yale ya benki. Nchini Tanzania kuna tasisi maarufu kama FINCA,Blue ,Branc na nyingine nyingi ambazo zinatoa mikopo ya biashara.
Mara nyingine utahitaji kuwa katika vikundi ili kupata mikopo kwa urahisi au kuwa na biashara iliyosajiliwa kisheria.
2. Mkopo Toka Kwa Ndugu, Jamaa Au Marafiki
Ndugu na Marafiki ni sehemu nyingine ambayo unaweza kufikiria unapohitaji mtaji wa biashara.
Ni watu wanaokupenda na kukuamini na wako tayari kukusaidia katika harakati zako za kufanikiwa kibiashara. Wako tayari kukusaidia kama wana uwezo wakufanya hivyo. Lakini bado wanahitaji uhakika kuwa fedha zao zitarudi. Watapenda kujua mpango wako na ni lazima uwe tayari kuwajulisha,sio tu kabla hata baada ya kupata mkopo ili wajue mwenendo wa fedha zao.
Kumbuka dhamana hapa haitakuwa mali bali uaminifu wako kwao. Ukishindwa kufanya ulichoahidi utavunja uhusiano wenu mzuri uliojengeka kwa muda mrefu.
Ni vyema kufikiria kwa makini kama utahitaji kuchagua njia hii,vinginevyo si njia nzuri sana.
3. Toka Katika Vikundi Vya Kuweka Na Kukopa
Vyama vya Kuweka na Kukopa vinatoa mikopo kwa wanacama wake. Katika vyama hivi wanachama wanatakiwa kuweka fedha katika akaunti zao. Mwanachama anaruhusiwa kukopa kulingana na kiasi alichoweka. Baadhi ya vyama vinaruhusu mwanachama kuchukua mkopo kufikia mara nne ya kiasi alichoweka. Mkopo huu huwa na riba ndogo ulilinganishwa na benki.
Pia masharti yake si magumu na ya hatari kama ya benki.
Kuna vikundi vingine vya kijamii ambavyo wanachama wamekuwa wakifanya hivyo na vinatoa fursa kwa wanachama kupata mitaji kwa kukopa.
Vikundi vya Kuchangiana:
Pia kuna mtindo wa kuchangiana kila mwezi ambapo wanachama katika kikundi watachanga kiasi fulani cha fedha na kumpa mmoja wao ili afanya kitu fulani muhimu ambacho asingeweza kwa kuwekeza binafsi.
4. Mtaji Toka Kwa Wawekezaji Binafsi Wa Nje
Kuna watu binafsi na makapuni ambayo tayari yanafedha na yanahitaji kuwekeza katika biashara yenye kupata faida ili fedha zao ziongezeke. Watu hawa wanaweka fedha benki ambako hazizai kwa riba nzuri kulinganisha na biashara.
Watu hawa wanahitaji taarifa za kutosha kuwashawishi kuwa fedha zao ziko katika mikono sahihi. Pia hata baada ya kuwekeza watahitaji taarifa za mara kwa mara juu ya maendeleo ya biashara. Kama biashara ni mbaya huenda wakatoa fedha zao ili wasipate hasara.
Hii ni sehemu nyingine ambayo huwa haiangaliwi sana na wajasiriamali wadogo kwani ile dhana ya kufanya biashara kwa kushirikiana bado haijakubalika na kufuatwa. Lakini njia hii inatoa nafasi kwa wale ambao wanabiashara yenye mfumo mzuri na inakosa mtaji tu kufanikiwa.
Lakini hata kwa biashara zinazoanza, kama kuna mpango mzuri na wazo lenyewe la bishara linaonyesha kufanikiwa basi wawekezaji hawa watakuwa tayari kuwekeza katika biashara yako.
Hii ni njia nzuri kwa wale wenye uwezo wa kubuni biashara nzuri zenye kutoa huduma kwa watu na yenye nafasi kubwa ya mafanikio lakini wanakosa fedha za kuanzia. Hawa wanaweza wakaanza hata bila kuwa na shilingi moja,mpango wa biashara pekee ndio wanachohitaji.
Kisha ongea na matajiri katika mji wako(angalia usitoe taarifa zote za mpango wako mpaka upate uhakika kuwa utapata fedha-kuzuia kuibiwa mawazo).
5. Uwekezaji Binafsi (Kuweka Akiba)
Inasemekana kuwa zaidi ya asilimia 50 ya bishara ndogo zonazoanzishwa huanza kutokana na akiba binafsi ya wamiliki.
Mmiliki kupitia nyenzo zilizopo za kupata kipato kama ni kazi au biashara nyingine iliyosimama tayari anaweka akiba maalumu kwajili ya kuanzisha biashara mpya. Kiasi cha kuanza kikifikiwa basi fedha hizo zinaingizwa katika biashara mpya.
Fedha hizi zinaweza zikaingizwa kama mkopo binafsi ambapo baadae zitarudishwa katika akaunti binafsi ya mmiliki au zikaingia kama uwekezaji katika biashara ambapo mmiliki atapata faida tu itakayozalishwa.
Vyovyote vile njia hii ni nzuri kwani hakuna madeni toka nje na unaweza ukawa na amani sana katika uendeshaji wake.
Kama wewe ni mwajiriwa na unafikiria kuwa na bishara yako basi njia hii ya kuweka akiba kwajili ya bishara yako ni njia sahihi.
Unaweza ukafungua akaunti nyingine nje na ile ya kawaida na kuhamisha asilimia fulani kila mwezi kwenda katika akaunti hiyo ya biashara (10-25% ni kiwango kizuri)
Ukitaka Mafanikio Ni Lazima Uchukue Hatua Za Haraka
Imesemwa kuwa usisubiri hadi kila kitu kikamilike ndio uanze,katika biashara hiyo inaweza kuwa ngumu au ikakufanya usianze kabisa.
Kama tayari una mpango wa bishara unaovutia usisite kuanza kwa kukosa mtaji,chagua njia mojawapo ya kupata mtaji na uanze.
Ukitaka kupanda jengo la ghorofa ndefu,anza ngazi ya kwanza na utajikuta uko juu .
Ukisubiri kufanya yote kwa mara moja huenda usifanye kabisa. Unapoanza kufanya kitu unapata urahisi kwa jinsi ambavyo unaenda mbele na njia inakuwa wazi kwako katika kila hatua unayochukua.
Mbinu 5 za kuanza na kukuza biashara kwa mtaji mdogo
1. Jipe muda, biashara haitaweza kukua haraka kama unavyofikiri
Uzuri wa kuanza biashara na mtaji kidogo ni kwamba kila mtu anaweza kufanya hivyo. Lakini pia urahisi huu wa kuanza biashara kwa mtaji kidogo unafanya ukuaji wa biashara kuwa wa taratibu sana. Hivyo unapofanya biashara yoyote ambayo unaanza na mtaji kidogo ni muhimu ukajipa muda ili kuweza kukuza mtaji wako. Usiwe na tamaa ya kutaka kukuza biashara hii haraka, unaweza kuingia kwenye maamuzi ambayo yatakugharimu zaidi. Endelea kufanya biashara yako huku ukijifunza zaidi na kuangalia kila fursa ambayo unaweza kuitumia kukuza biashara yako.
2. Kuza mtaji wako taratibu
Kwa mtaji huo mdogo ambao umeanza nao biashara, endelea kuukuza kila siku. Usiendeshe biashara kwa kula kila kipato unachopata, badala yake tenga sehemu ya akiba irudi kwenye biashara yako. Fanya hivi kwa nidhamu ya hali ya juu sana na unahakikisha kila unapopata faida sehemu inarudi kwenye biashara yako. Pia endelea kuangalia kwa mazingira uliyonayo na kwa biashara unayofanya ni kwa jinsi gani unaweza kukuza mtaji wako zaidi. Kama utafikiria hili kila siku, hutakosa majibu ambayo yatakusaidia.
3. Punguza gharama za biashara na za maisha pia
Kuwa kwenye biashara haimaanishi kwamba ndio una uhuru wa kufanya chochote unachotaka na fedha za biashara hiyo, kwa sababu tu ni zako. Wewe sasa upo kwenye wakati mgumu wa kukuza biashara yako huku ukiwa huna njia nyingi za kufanya hivyo. Hebu kwa sasa punguza kabisa gharama zako za kibiashara na za maisha pia. Kama kitu sio muhimu sana basi usikigharamie. Punguza matumizi yote ambayo ni ya anasa tu na sio kwa ukuaji wa biashara. Katika kupunguza gharama zako za biashara na maisha, jijengee nidhamu nzuri sana ya fedha. Usitumie fedha kiholela tu, kuwa na mahesabu na sababu kwa nini umetumia fedha fulani, hasa kwa matumizi ambayo sio ya kawaida.
4. Angalia watu ambao unaweza kushirikiana nao
Baada ya kuiendesha biashara yako vizuri na ukaona inaenda kwa faida, unaweza kuangalia watu ambao unaweza kushirikiana nao kwenye biashara hiyo. Kuna watu wengi ambao wanaweza kuwa na mtaji lakini hawana muda wa kufanya biashara. Lakini pia watu hawa wanataka mtu ambaye wanaweza kumwamini. Hivyo kama unaweza kuaminika angalia watu unaoweza kushirikiana nao kibiashara. Andaa mpango mzuri ambao utamshawishi mtu ni jinsi gani yeye atafaidika kama atawekeza kiasi kidogo kwenye biashara yako. Ikiwa unaendesha biashara yako kitaalamu itakuwa rahisi zaidi kushawishi watu kushirikiana na wewe.
5. Rasimisha biashara yako ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kupata mkopo
Hata kama biashara yako ni ndogo kiasi gani, irasimishe. Iendeshe kisheria kwa kuwa na namba ya mlipa kodi na hata leseni pia. Hivi vitakuwezesha wewe kutambulika na taasisi za kifedha pale utakapohitaji msaada zaidi wa kifedha. Mkopo kwenye taasisi za kifedha ni chanzo muhimu ila usikimbilie kama bado hujaweza kuiendesha biashara yako kwa faida. Hakikisha umeiweka biashara yako vizuri kwanza na inajiendesha kwa faida ili unapochukua mkopo unajua unauweka wapi na kuendelea kupata faida zaidi.
Kuikuza biashara pale ambapo umeanza na mtaji kidogo ni kitu ambacho kinawezekana. Ila unahitaji kujitoa na kujenga nidhamu kubwa. Unahitaji kufanya kazi zaidi ya wafanyabiashara wengine, unahitaji kuwa mbunifu wa hali ya juu na pia unahitaji kujijengea uaminifu. Ukishajua wewe biashara yako ni ndogo na inahitaji kukua, basi hakikisha kila mara unaumiza akili yako ifikirie njia zaidi za kuikuza. Na kama utaweza kufanya hivi basi utaziona fursa nyingi zilizokuzunguka za kuikuza biashara yako.
Kama Wewe Ni Mjasiriamali, Acha Kabisa Kuogopa Mambo Haya
Kila mtu katika maisha yake anataka kufanikiwa. Kutokana umuhimu huu wa mafanikio kila mtu hujikuta akiweka juhudi kwa kile anachokifanya ili kufikia mafanikio hayo. Lakini pamoja na juhudi zote hizo wengi wetu huwa wanashindwa kufikia mafanikio hayo kutokana na kuogopa mambo fulani fulani ambayo hawakutakiwa kuyaogopa kabisa.
Kwa kuyaogopa mambo hayo na kuyakuza husababisha kushidwa kufikia mafanikio. Hili ndilo kosa kubwa ambalo wengi wamekuwa wakifanya kwa kuogopa kitu ambacho hawakutakiwa kukiogopa na matokeo yake husababisha kushindwa kufanya kitu ama kuchukua hatua. Kama wewe ni mjasiriamali na unayetaka mafanikio makubwa acha kuogopa kabisa mambo haya:-
1. Kushindwa.
Mjasiriamali yoyote mwenye nia ya kufika kwenye kilele cha mafanikio siku zote haogopi kushindwa. Kama ameshindwa katika jambo hili atajaribu hili na lile mpaka kufanikiwa. Lakini siyo rahisi kuacha njia ya mafanikio eti kwa sababu alishindwa kwa mara ya kwanza. Hiki ni kitu muhimu sana kukijua katika safari yako ya mafanikio ili we mshindi.
SOMA; Mambo 6 Unayolazimika Kuyaacha Mara Moja Ili Kufanikiwa.
2. Kukosolewa.
Watu wenye mafanikio siku zote hawaogopi kukosolewa. Hawa ni watu wa kufanya mambo ambayo wanaamini yatawafanikisha na siyo kinyume cha hapo. Kama ikitokea utawakosoa, wao mara nyingi hawajali sana, zaidi wanashikilia misimamo yao. Kitu cha kujifunza hapa, acha kuumia sana na kukosolewa kwako. Amini unachokifanya kisha songa mbele.
3. Mafanikio ya wengine.
Siku zote wajasiriamali wa kweli hawagopi mafanikio ya wajasiriamali wengine. Wanajua mafanikio ni hatua na wao watafika huko tu. Hivyo hawatishiki sana, zaidi wanafuata mipango na malengo yao mpaka kuifanikisha. Kutokuogopa mafanikio ya wengine ni silaha kubwa sana ya kutufikisha hata sisi kwenye kilele cha mafanikio hayo, ila kwa kujiamini.
4. Kuacha kile unachokifanya.
Mara nyingi ili ufanikiwe ni lazima uwe king’ang’anizi. Sasa inapotokea mambo hayaendi sawa kama unavyotaka hakuna njia nyingine zaidi ya kuacha kile unachokifanya. Wajasiriamali wenye mafanikio makubwa huwa siyo waoga sana kuacha vile wanavyofanya. Lakini hufanya hivyo mpaka wakishagundua hakuna mafanikio wanayaona kabisa na siyo kuacha kirahisi tu.
5. Kutengeneza pesa nyingi.
Ili uweze kufanikiwa zaidi ni lazima ujue umuhimu wa kutengeneza pesa zaidi. Ikiwa unataka kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa acha kabisa kuogopa kutengeneza pesa zaidi na zaidi tena na zaidi. Inapotokea fursa ya kutengeneza pesa itendee haki kwani huo ndio msingi wa mafanikio yako makubwa ambayo unayatafuta.
6. Kujifunza.
Hauwezi kufanikiwa kwa viwango vya juu bila kujifunza. Wajasiriamali wote wenye mafanikio makubwa ni watu wa kujifunza kwenye maisha yao. Na hujifunza kupitia wenzao waliofanikiwa au kupitia vitabu. Huu ndiyo ujasiri walionao katika hili na hawaogopi kitu. Inapotokea kuuliza, wanauliza mpaka kufanikiwa.
Unaweza ukajifunza mengi na kuyashangaza ambayo watu wenye mafanikio hawaogopi kuyafanya katika maisha yao. Chukua hatua yakubadili maisha yako na kuanzia sasa amua kuwa miongoni mwa wana mafanikio.
Kabla Ya Kufanyia Kazi Ushauri Wa Kibiashara Unaopewa, Zingatia Haya
Kama kuna kitu ambacho kila mtu anaweza kushauri kadiri ya utashi wake, basi ni ushauri wa kibiashara. Watu wengi wamekuwa wakipokea ushauri wa biashara unaotolewa na kila mtu, tena kwa bure, lakini wanapoufanyia kazi ndipo wanagundua haukuwa ushauri mzuri.
Kila kipindi kuna aina za biashara ambazo huwa zinashabikiwa na watu wengi, biashara ambazo kila mtu anaongelea na wale wanaozifanya kuonekana waipata faida. Hapa ndipo unakuta kila mtu anashauriwa kuingia kwenye biashara hiyo, kwa sababu ndiyo ‘habari ya mjini’ kwa wakati huo na hivyo wengi wanakimbilia kuchukua hatua kabla fursa haijawapita.
Changamoto nyingine kubwa inayowafanya watu kupewa ushauri ambao siyo makini kwenye biashara ni kutokuwa tayari kulipa gharama za ushauri. Wengi wamekuwa wakichukulia ushauri kama kitu kidogo ambacho hakipaswi kulipiwa. Hivyo wanachukua ushauri wa bure ambao unawaumiza sana.
Leo tutakwenda kujifunza mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kufanyia kazi ushauri wowote unaopewa kibiashara. Kwa kuzingatia mambo haya utaepuka kufanya maamuzi ya msukumo ambayo yatakuingiza kwenye hasara.
Jambo la kwanza; fanya utafiti wako mwenyewe.
Usipokee maneno ya watu na kuyaamini kwa asilimia mia moja. Fanya utafiti wako kujua kama kweli biashara unayoambiwa inalipa kama ni kweli. Angalia ukubwa wa soko la biashara hiyo, ona ni kwa kiasi gani bado wateja hawajafikiwa. Pia angalia uwezekano wa kukua zaidi kwenye biashara hiyo. Fanya utafiti wako mdogo kulijua soko na hata kuwajua wale waliopo kwenye biashara hiyo kwa sasa.
Jambo la pili; ongea na wale wanaofanya.
Kwa kuwa umesikia biashara inalipa, usifikiri kwamba haina changamoto zake. Na ili kujua changamoto za biashara yoyote, angalia wale ambao wanafanya biashara hiyo. Ongea nao au wafuatilie ili kuona changamoto yao hasa ni nini. Ni vyema ukazijua changamoto za biashara yako mapema kabla hata hujaingia ili uweze kupambana nazo.
Wengi wa wanaoshindwa kwenye biashara mpya ni kutokana na kukutana na changamoto ambazo hawakuzitegemea hapo awali.
Jambo la tatu; mwangalie yule anayekupa ushauri wa biashara.
Watu wengi wamekuwa wakitaka kusikia tu ushauri mzuri wa biashara, hivyo wakiusikia hawajali anayewaambia ni nani. Hivyo unakuta mtu kasikia wengine wanasema biashara fulani inalipa, na yeye anatoka na taarifa hizo kuja kukupa wewe. Hajafanya utafiti wowote na wala hana utaalamu wa biashara, ila amesikia inalipa na anakuambia na wewe ukafanye kwa sababu inalipa.
Hakikisha mtu unayechukua ushauri wa biashara kwake ana utaalamu wa biashara au anafanya biashara hiyo anayokushauri ufanye. Kama na yeye amesikia inalipa ila hajui kwa kina kuhusu biashara hiyo, ni vyema ukaokoa muda wako au kufanya utafiti zaidi kabla hujaingia kwenye biashara hiyo.
Ni rahisi kushauri kuliko kufanya, hivyo mara zote unapopokea ushauri chunguza kwa makini kabla hujachukua hatua. Usiharakishe kufanyia kazi ushauri unaopewa kwa sababu tu unaonekana ni biashara itakayokulipa. Fanyia kazi ushauri unaopewa na utoke na mpango ambao unaweza kuupigania mpaka kufanikiwa kwenye biashara yako.
Mambo Matano Ya Kuzingatia, Kama Wewe Ni Mjasiriamali Unayetaka Mafanikio Makubwa
Mafanikio ni kitu cha lazima sana katika safari ya mjasiriamali. Uwe mjasiriamali mdogo, wa kati au mkubwa kwa vyovyote vile unahitaji mafanikio. Lakini ili kufanikiwa na kufikia mafanikio hayo, yapo mambo ya msingi ambayo unatakiwa kuyazingatia. Mambo hayo ni kama haya yafuatayo:-
1. Kujiwekea malengo.
Ukiwa kama mjasiriamali unayetakiwa kufikia mafanikio makubwa, suala la kujiwekea malengo ni lazima kwako. Unapokuwa na malengo yanakuwa yanakupa mwelekeo sahihi wa kupata kile unachokitaka. Hiki ni kitu ambacho unahitaji kukizingatia sana kwani ni nguzo kubwa ya kufikia mafanikio makubwa.
2. Kujitoa Mhanga(Take Risks)
Hakuna mafanikio makubwa utakayoyapata bila kujitoa mhanga. Wajasirimali wote wakubwa ni watu wa kujitoa mhanga sana. Wanakuwa wako tayari kutoa kitu chochote ilimradi wafikie malengo yao. Kitu cha kuzingatia hata kwako wewe unalazimika kujitoa mhanga na kulipia gharama ili kufikia mafanikio makubwa.
3. Kutokuogopa Kushindwa.
Wengi wetu tumefundiswa sana kuwa kushindwa ni vibaya. Hali ambayo hupelekea tunakuwa tunaogopa kujaribu karibu kila kitu kwa sababu ya hofu ya kushindwa. Ikiwa wewe ni mjariamali unatakiwa kuwa jasiri na kujua kwamba mafanikio yanataka roho ya ujasiri na kutokuogopa kushindwa. Hiyo ndiyo siri itakayokifikisha kwenye kilele cha mafanikio na sio uoga unaouendekeza.
4. Acha kuridhika mapema.
Ni kosa kubwa sana kujikuta unaridhika mapema eti tu kwa sababu ya faida unayoitengeneza sasa. Ni vizri kujua, safari ya mafanikio bado ni ndefu kwako, hivyo hutakiwi kuridhika kwa namna yoyote ile. Kama kuna jambo umelifanikisha, endelea kwenye jambo lingine hadi kujenga mafanikio makubwa kabisa.
5. Tafuta ‘Mentor’
Acha kujidanganyai kuingia kwenye safari ya mafanikio huku ukiwa peke yako. Ikitokea umekwama kwa sababu huna mtu wa kukuelekeza au kukushauri, huo ndiyo unakuwa mwisho wako. Hivyo ni muhimu kuwa na kiongozi wako ‘mentor’ ambaye atakuongoza kwenye kufikia mafanikio yako.
Kwa kuyajua mambo hayo yatakusaidia wewe mjasiriamali kuweza kuendelea mbele zaidi na kufanikiwa katika safari yako yamafanikio.
Biashara Unazoweza Kuanza Kwa Mtaji Wa Tsh Laki Mbili Na Kuweza Kufanikiwa.
Kabla sijamshauri msomaji mwenzetu kuhusu biashara gani afanye, kuna mambo muhimu nahitaji ayajue na kuyazingatia sana kwenye biashara yoyote atakayokwenda kufanya;
1. Kwa kuanza biashara na mtaji kidogo atahitaji kuweka juhudi kubwa sana kwenye uendeshaji wa biashara hiyo.
Kadiri biashara inavyoanza kwa mtaji kidogo, ndivyo uendeshaji wake unavyokuwa mgumu na changamoto zinakuwa nyingi. Hivyo mtu unapoingia kwenye biashara kwa mtaji kidogo unatakiwa kujiandaa kiasi cha kutosha. Utahitajika kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja, kitu ambacho kitakuchosha sana.
Pia unatakiwa kuelewa kwamba kwa kuanza biashara na mtaji kidogo itakuchukua muda mrefu zaidi mpaka kufikia yale mafanikio ambayo umepanga kuyafikia kibiashara.
Ni muhimu kujiandaa kwa hili ili mambo yanapokuwa magumu usikate tamaa, badala yake ujue ndiyo kitu ulichotegemea kukutana na cho na hivyo kuongeza juhudi zaidi.
2. Biashara haijali umetokea wapi au umepitia magumu kiasi gani.
Msomaji mwenzetu ametueleza changamoto alizopitia na maisha ya chini ambapo ametokea. Hii ni nzuri katika kuweka maelezo yako ya kuomba ushauri, lakini ni kitu cha kuweka mbali pale unapoanza biashara. Watu wengi wamekuwa wakifikiri kwamba kwa sababu wamepitia maisha magumu basi biashara inapaswa kuwa rahisi kwao. Unachotakiwa kujua ni kwamba biashara haijali umetokea wapi au umepitia mambo magumu kiasi gani.
Biashara itakuja na changamoto zake kama ilivyo kwa watu wengine. Hivyo unahitaji kuweka hadithi yako ngumu pembeni na kujiandaa kupambana na biashara. Usiingie kwenye biashara ukiwa mnyonge, ingia ukiwa unajiamini ya kwamba unaweza kufanya makubwa na hupo tayari kukata tamaa hata kama mambo yatakuwa magumu kiasi gani.
3. Huna uhuru mkubwa wa kuchagua.
Unapoanza biashara kwa mtaji kidogo, huna uhuru mkubwa wa kuchagua ni biashara ya aina gani unataka kufanya, badala yake unahitaji kuingia kwenye biashara yoyote ambayo inaweza kukuletea faida mapema. Ukishapata biashara ya aina hii unaweka juhudi zako na biashara inapokua ndipo unaanza kuwa na uhuru wa kuingia kwenye zile biashara ambazo unazipenda.
Biashara unazoweza kuanza na mtaji kidogo wa tsh laki mbili.
Kwa msingi huo ambao tumeujenga hapo juu sasa tuangalie biashara ambazo msomaji mwenzetu anaweza kuzianza na mtaji kidogo wa laki mbili. Kuna biashara nyingi ndogo ndogo hasa kwa maeneo ya mjini kama dar es salaam ambazo mtu anaweza kuanza kwa mtaji usiozidi laki mbili. Unaweza kuangalia kwenye eneo ulilopo watu wana changamoto gani au mahitaji gani ambayo ni makubwa na kuweza kuwasaidia watu kuyatimiza.
Zifuatazo ni baadhi ya biashara ambazo mtu anaweza kuanza kwa mtaji kidogo kwa dar es salaam.
1. Kuuza nguo kwa kutembeza mitaani.
Hii ni biashara ambayo unaweza kuianza kwa mtaji kidogo. Kwa biashara hii unahitaji kwenda kwenye masoko makubwa ya nguo au viatu, iwe ni mtumba au ‘special’ chagua nguo nzuri na kisha kuzunguka mitaani kuuza nguo hizo. Kadiri unavyopata nguo nzuri na jinsi unavyoweza kuwa na kauli nzuri ndivyo unavyoweza kufanya mauzo makubwa. unahitaji kuweza kuongea vizuri na watu, na kuwa na ushawishi kwa nini mtu anunue. Nguo za wanawake na watoto zina wateja wengi zaidi ukilinganisha na za wanaume.
2. Kuuza genge au matunda.
Biashara nyingine ambayo mtu anaweza kuianza kwa mtaji kidogo ni kufungua genge la mahitaji ya msingi ya nyumbani kama mboga mboga au kuuza matunda. Haya ni mahitaji ya msingi sana ambayo bado wengi hawayapati vizuri. Kama ukiweza kupata bidhaa zilizo bora na kuwauzia watu kwa bei nzuri wanayoweza kumudu, unaweza kutengeneza biashara nzuri. Na kama kwa fedha kidogo uliyonayo haikutoshi kukodi eneo la kuuzia unaweza kuja na mbinu mpya ya kuuza kwa mfano kuwa na mkokoteni mdogo ambao unazunguka nao mtaa kwa mtaa kuuza bidhaa zako.
3. Kutoa huduma za maji safi kwa maeneo ambayo maji bado ni tatizo.
Kuna maeneo mengi ya dar es salaam ambapo watu bado hawapati maji masafi. Au maji hayo yanapatikana mbali na hivyo wengi kushindwa kuyapata, unaweza kutumia fursa hii kuwasambazia watu maji masafi. Unahitaji kuwa na mkokoteni na madumu yako ya maji, kujua eneo ambapo utapata maji safi na kuweza kuwasambazia wateja wako.
4. Kubeba takataka kutoka kwenye makazi ya watu.
Licha ya kuwepo kwa mifumo ya uzoaji taka kama magari na majalala makubwa, bado watu wengi hawafikiwi au hawatumii mifumo hii. Hivyo hapa kuna fursa ambapo mtu unaweza kuingia na kufanya biashara. Unahitaji kuwa na mkokoteni ambao unaweza kubeba taka na unahitaji kujua sehemu ya kwenda kuzimwaga. Hapa unaweza kupita kwenye mitaa, nyumba kwa nyumba na kuwapatia huduma ya kuzoa taka zao kwa bei ambayo wanaweza kuimudu.
Hizo ni baadhi ya biashara unazoweza kuanza kuzifikiria na hata kuzifanya. Unaweza kuchagua moja na kuiboresha zaidi kulingana na mazingira uliyopo. Au unaweza kufikiria biashara nyingine kwa mazingira ambayo upo. Kikubwa usianze kuchagua na kuona kuna biashara inayokufaa au ipi haikufai, unapoanza biashara kwa mtaji mdogo huna nafasi kubwa ya kuchagua.
Njia 5 za Kukabiliana na Madeni Katika Maisha
Huenda ukawa unadaiwa madeni mengi na unaona nivigumu kwako kukabiliana nayo moja kwa moja, usiogope jaribu njia mbadala za kuweza kukabiliana na madeni hapa.Zifuatazo ni baadhi ya njia zitakazo kusaidia kupambana na ulipaji wa madeni .
1: Tengeneza Orodha yote ya madeni unayodaiwa.
Unapaswa kufahamu madeni yote unayodaiwa na umjue mtu, kikundi au kampuni inayokudai.Kufanya hivyo kutakukumbusha kujipanga vizuri katika swala zima la ulipaji.
2: Panga madeni yako kulingana na kiasi, umuhimu na uharaka wa kuyalipa.
Yapatie kipau mbele yale madeni uhimu yanayoweza kukuchukulia hatua mara moja.Mara nyingi madeni haya huwa ni ya kawaida, kwa mfano; kodi ya nyumba, kusimamishiwa huduma muhimu(maji, umeme) Ada ya shule au hata kwenda jela.Lakini sii lazima uanze tu na madeni ya aina hii, bali inategemeana na hali iliyopo.
3: Tengeneza bajeti yako peke yako.
Fanya mahesabu ili kujua kipato ulichoingiza kwa wiki au mwezi, pamoja na gharama zake zote, hii itakusaidia sana kuokoa pesa zako.Bajeti itakusaidia kuamua nini unaweza kumudu kulipa wadai wako, hivyo ni muhimu kuwa mkweli.
4: Kuwa mkweli na muwazi kwa wadeni wako.
Watu wengi wanafikili kumkwepa mdeni wake ndiyo njia pekee ya kukabiliana na madeni, hapana! mara nyingi hii hukujengea taswira mbaya katika jamii unayoishi nayo.Nivyema ukapokea simu ya mdeni wako na kumwambia ukweli na kuomba akuongezee muda wa kuweza kujipanga zaidi na kufanikisha kulipa madeni yako.
5: Tumia njia ya mazungumzo baina yako na mtu anaye kudai.
Nivyema ukakubaliana na mdeni wako kias na jinsi ya kulipa deni, nakama ikishindikana baadaya kuwa umeshakopa, tafuta ushauri kwa wataalam, watakusaidia jinsi ya kulipa madeni, kwa mfano taasisi binafsi zinazohusika na mikopo katika jamii.Nivyema ukakabiliana na madeni yako moja kwa moja- kwasababu jinsi upuuzavyo kulipa madeni ndivyo hali itakavyozidi kuwa mbaya kwako.
NB
Kamwe usikimbie madeni, jitahidi ukabiliane na madeni kwa kutumia lugha nzuri kwa mdeni wako, kwasababu madeni humkosesha mtu uhuru, amani na hata pia huhatarisha maisha.Asante!
Sababu Sita(6) Zinazoweza Kumpoteza Mteja Au Kumkera Katika Biashara
Muda mwingine unaweza ukajiuliza kwa nini mteja au wateja Fulani siku hizi huwaoni katika biashara yako, unaanza kumtafuta mchawi ni nani katika biashara yako kumbe mchawi ni wewe mwenyewe ambaye unaweza ukawavuta wateja wengi au mteja au ukaongeza mteja ,wateja katika biashara yako hii inatokana tu na jinsi gani unatoa huduma yako na kumhudumia mteja pia.
Leo tutaangalia ni sababu gani ambazo zinaweza kusababisha kumpoteza au kumkera mteja wako nazo ni;
1. Kuchelewa Kufungua Biashara
Kuna baadhi ya wamiliki wa biashara wanachelewa kufungua biashara na unakuta mteja anahitajia kupata huduma mapema ukilinganisha na muda wako ambao unafungua biashara sababu hii inaweza ikampoteza mteja au kumkera kama tabia yako wewe kila siku ni kuchelewa mteja anakusubiri katika eneo la biashara badala ya wewe kumsubiri mteja sababu inaweza ikapelekea kumkera au kumpoteza mteja wako.
2. Kufanya Biashara kwa Mazoea/ Kujisikia
Unapokuwa umeamua kufanya biashara basi fanya kila siku bila mazoea au kujisikia kuna wafanyabiashara wengine wanafanya biashara kwa kujisikia au kwa mazoea kwa mfano, leo anaweza kufungua kesho kafunga sasa tabia kama hii inaweza kumsababishia mteja kupata kero na kukuhama kabisa ukiamua kufanya biashara fanya kila siku bila kukata tama bila kujali siku yaani siku Fulani kuna wateja na siku Fulani hakuna wateja hivyo basi unaamua kutofanya biashara kwa hiyo acha kufanya biashara kwa mazoea.
3. Kuacha Biashara peke yake
Kuna tabia ya wafanyabiashara wanaweza kufungua biashara yao na kuacha peke yake anazungukazunguka au kwenda sehemu kupiga stori huku akiacha biashara yake wazi mteja akija anapata shida ya kumtafuta mtoa huduma unafikiri kama kuna sehemu nyingine ambapo mteja huyu anaenda na kumkuta mtoa huduma yuko katika eneo lake la biashara kila siku je ataweza kushawishika tena kurudi kwako? Kama sehemu nyingine anahudumiwa vizuri?
4. Kuwa na Lugha/Kauli mbaya
Unapokuwa unafanya biashara unatakiwa uwe na kauli nzuri ambazo zitamvutia mteja kuja kwako kupata huduma. Kuna wateja wengine ndio wanaweza kuwa na kauli mbaya lakini wewe hupaswi kuwa na kauli mbaya hupaswi kumjibu kwa lugha mbaya soma saikolojia ya mteja au wateja wako muudumie kwa upendo, kwa ukarimu wa hali ya juu ili siku nyingine arudi tena kwako. Kwa hiyo kauli mbaya ni moja ya sababu ambazo zinaweza kukuletea matokeo hasi katika biashara yako. Chunga sana ulimi wako katika biashara.
5. Kutopenda Biashara yako
Kuna wafanyabiashara wengine wanatoa huduma kama vile wamelazimishwa kufanya biashara hiyo. Kutopenda kazi yako ni moja sababu zitakozomfanya mteja naye asivutiwe na biashara yako. Kuwa na uso wa furaha mchangamkie mteja ongea naye vema katika lugha ya ushawishi onesha jinsi gani unaipenda kazi yako, unafanya kwa moyo na juhudi zote huwezi kumpoteza mteja wako. Kwa hiyo ili ufanikiwe katika jambo Fulani penda kwanza hicho unachokifanya kwa moyo wote.
6. Kubadilisha bei mara kwa mara.
Katika kila bidhaa unayouza mfano duka kuna kuwa na bei elekezi ya vitu unavyouza kwa bei ya jumla au rejareja. Sasa kuna baadhi ya wafanyabiashara wanauza kwa bei ya juu sana ili kupata faida ya juu hapa unakuwa unamlangua mteja na kumkatisha tamaa tena ya kurudi kwako kupata huduma, kwa hiyo unapofanya biashara usiwe mtu wa kubadilisha bei mara kwa mara leo mteja akija bei nyingine kesho bei nyingine itamfanya akose imani na wewe na kukukimbia kabisa.
Hatua 26 za Kufuata Katika Kuanzisha Biashara Ndogondogo
Zifuatazo ni hatua 26 za kufuata katika kuanzisha biashara ndogondogo ambazo zitakuwezesha wewe kuanzisha biashara yeyote kwa uraisi zaidi.
Hatua ya kwanza ikiwa imebeba hatua zote kwani biashara inahitaji utayari (kuamua) zaidi ya vitu vingine kama mtaji nk
Hatua ya ya 1: Kuamua kuingia katika biashara
Kuamua kuingia katika biashara ni majumuisho ya utayari wa kisaikolojia, kiakili, kiuchumi na kukabiliana na hatari au vitisho vyote vitakavyojitokeza kwenye biashara
Maamuzi yako na hasa maamuzi magumu juu ya aidha kufanya hiyo biashara au la si ile hali ya kuamua kufanya biashara tu, bali pia ni ile hali ya kukubaliana na ups and downs za biashara husika na kuwa tayari kujitoa mhanga zaidi.
Hatua ya 2: Kuchanganua uwezo na udhaifu wako
Maeneo manne ni muhimu yapatiwe taarifa halisi na kuchukua hatua ili uweze kumudu kufanya biashara husika
Mazingira wezeshi Mazingira pingamizi
Mazingira ya Ndani UwezoUwezo wako katika kuendesha biashara mfano: utaalam, vitendea kazi, kiwanja nk. UdhaifuUdhaifu wako katika kuendesha biashara mfano: ukosefu wa utaalam, vitendea kazi, kiwanja nk.
Mazingira ya Nje FursaKuwepo kwa sera nzuri, katiba nzuri, hali ya hewa nzuri, mwitikio wa jamii nk VitishoKutokuwepo kwa sera nzuri, katiba nzuri, hali ya hewa nzuri, mwitikio mbaya wa jamii nk
Hatua ya 3: Kupata mafunzo
Baada ya kujua udhaifu wako, pata mafunzo
Mfano:- Ya kupata ufundi au kubadili mitizamo
Kupata utaalam wa kiufundi katika biashara husika
Hatua ya 4: Kupeleleza mazingira utakayofanya biashara
Ni lazima upeleleze ili ujue fursa na hatari zilizopo katika biashara hiyo. mfano hatari (Risks, constraints) zaweza kuwa ni sheria na sera mbaya za nchi, sheria na sera kandamizi za kimataifa, barabara mbovu, hali ya hewa mbovu nk. Unatakiwa kusijua zote hizo ili aidha uweze kuzikwepa au kuzikabili.
Fursa nzuri zilizopo zaweza kuwa ni sheria na sera nzuri, miundo mbinu nzuri, nk
Hatua ya 5: Kuchagua biashara gani ufanye
i) Kuzalisha bidhaa (Manufacturing)
ii) Kuchuuza (Kuuza bidhaa)
iii) Kutoa huduma (Service)
Kuzalisha bidhaa
Kuzalisha bidhaa ni kutumia rasilimali watu na malighafi ili kutengeneza bidhaa ya kuuza kwa mlaji au mchuuzi. Bidhaa ni kama vyakula, vyombo, nk
Kuuza bidhaa (Trading)
Kuchuuza bidhaa zilizotengenezwa na wengine ili kupata faida. Unaweza uza moja kwa moja kwa mlaji au ukauza kwa jumla (whole sale)
Kutoa huduma (Service)
Kutumia ujuzi wako au wa wengine katika kuwahudumia watu na shida zao kwa malipo. Mfano kufundisha, kutibu, kusafirisha, kutumbuiza nk
Hatua ya 6: Utafiti wa soko (Market Survey)
Washindani wako, uwezo na udhaifu wao
• Ukubwa wa soko
• Mgawanyo wa soko
• Aina ya soko/masoko
• Tabia za soko
• NK
Hatua ya 7: Mfumo wa biashara
Fuatilia maelezo ya kila mfumo ukitilia maanani faida na hasara za kila mfumo. Unaweza pia kumtumia mshauri wa masuala ya biashara kukushauri kulingana na mazingira yako utakayofanyia biashara.
Hasa unatakiwa kujua zaidi mambo ya kisheria katika mfumo utakaoamua kuutumia kuendehsa baishara yako ili isije ikakuletea shida huko mbeleni, maamuzi ya mfumo upi uuchukue inategemea zaidi sheria za ndani ya nchi husika, pia inategemea ukubwa wa mtaji wako nk.
Mtu mmoja (sole proprietor)
Faida yake
Kuanzisha ni rahisi
Maamuzi hupitishwa kwa haraka kwa hiyo hakuna urasimu
Hasara yake
Biashara ikipata shida mmiliki anahusika na hasara kama vile ya ufilisi nk
Ushirika (>watu wawili) (partnership)
Faida yake
Kuanzisha ni rahisi
Maamuzi hupitishwa kwa haraka kwa hiyo hakuna urasimu
Hasara yake
Biashara ikipata shida wamiliki wanahusika na hasara kama vile ya ufilisi nk
Mikataba inayoingiwa na mmoja wa washirika huwabana na wengine wasiohusika
Kampuni ya umma (public companies)(zaidi ya watu wawili bila ukomo)
Faida yake
Utambulisho wa kisheria
Ukomo wa ufilisi upo kwenye kampuni husika na sio wenye hisa
Ni rahisi kuvutia mitaji mikubwa kupitia masoko ya hisa
Hasara yake
Haina usiri hivyo ni hatari kwani washindani wa biashara husika wanaweza kutumia taarifa hizo kujipanga
Muda na rasilimali muda kupotea kwa shughuli za kihasibu na kazi za makaratasi
Kampuni ya binafsi yenye ukomo wa hisa
(private companies limited by shares) (watu wawili hadi 50)
Faida yake
Utambulisho wa kisheria
Ukomo wa ufilisi upo kwenye kampuni husika na sio wenye hisa
Kazi za makaratasi ni chache ukilinganisha na makampuni ya umma
Mlolongo wa taratibu za kisheria ni chache ukilinganisha na makampuni ya umma
Hasara yake
Gharama katika kuanzisha tofauti na biashara binafsi
Huruhusiwi kuuza hisa katika masoko ya hisa
Kampuni li lazima angalau iwe na wakurugenzi, katibu na mhasibu
Ni lazima ifanyiwe ukaguzi wa mahesabu kila mwaka
Kampuni ya binafsi yenye ukomo wa udhamini
(private companies limited by guarantees) (watu wawili hadi 50)
Faida yake
Utambulisho wa kisheria
Ukomo wa ufilisi upo kwenye kampuni husika na sio wenye hisa
Kazi za makaratasi ni chache ukilinganisha na makampuni ya umma
Mlolongo wa taratibu za kisheria ni chache ukilinganisha na makampuni ya umma
Hasara yake
Gharama katika kuanzisha tofauti na biashara binafsi
Huruhusiwi kuuza hisa katika masoko ya hisa
Kampuni li lazima angalau iwe na wakurugenzi, katibu na mhasibu
Ni lazima ifanyiwe ukaguzi wa mahesabu kila mwaka
Jumuiya (association)
Faida yake
Utambulisho wa kisheria
Inavutia wahisani
Ni ya watu wachache waliokubaliana
Hasara yake
Ukiritimba katika kupitisha maamuzi
Ugomvi wa mara kwa mara
Haina kinga kwa waazilishi
Vyama vya ushirika
Faida yake
Utambulisho wa kisheria
Inavutia wahisani
Ni ya watu wachache waliokubaliana
Hasara yake
Ukiritimba katika kupitisha maamuzi
Ugomvi wa mara kwa mara
Haina kinga kwa waazilishi
Mashirika yasiyo ya kiserikali
Faida yake
Utambulisho wa kisheria
Inavutia wahisani
Ni ya watu wachache waliokubaliana
Hasara yake
Ukiritimba katika kupitisha maamuzi
Ugomvi wa mara kwa mara
Haina kinga kwa waazilishi
Ukishachagua mfumo mzuri wa biashara yako, unatakiwa kuanza mchakato wa kuisajili katika mamlaka ya usajili wa makampuni inayoitwa BRELA ambayo ofisi zake zipo Jengo la shirika –Dar es salaam
Hatua ya 8: Kuchagua sehemu ya biashara
Kama ni sheli itabidi iwekwe kando ya barabara yenye magari mengi
Hatua ya 9: Kuchagua teknolojia
Ni muhimu kuangalia, kama biashara yako inategemea kwa ukubwa wake teknolojia usiende haraka hapa, tumia wataalamu wa technolojia husika ujua pro and cons zake kwani ukiharakisha hapa utaingia gharama isiyotakiwa na kuibebesha biashara yako mzigo wa manunuzi ambao hazikutakiwa, lakini pia technolojia husika inaweza kuchangia katika kupata faidi kubwa au hasra kubwa. uwe makini hapa.
Teknolojia itasaidia kujua
a) Aina ya watumishi
b) Aina ya vitendea kazi mashine /mitambo
Mfano kilimo cha maksai na kukamua kwa mashine
Teknolojia nzuri ni lazima iwe na sifa zifuatazo
a) Ni rahisi kutumiwa
b) Iwe rahisi kupata msaada kama mafundi nk
c) Iwe inaendana na tamaduni husika
d) Iwe ni rafiki wa watu na mazingira
e) Iwe na gharama ndogo za uendeshaji
f) Inaendelezeka
Hatua ya10: Kununua mashine na vifaa
Mashine na mitambo mingine itategemea sana uchaguzi wa teknolojia hapo juu 8(i)
Mashine zote na mitambo ni lazima kuzingatia yaliyotajwa hapo juu 8(ii)
Hatua ya 11: Usajili wa biashara
Hii hufanywa mara nyingi kwenye manispaa husika. Leseni kwa wafanya biashara ndogondogo ni bure (biashara ndogondogo ni ile ambayo mauzo yake hayazidi Shs 20 milioni kwa mwaka)
Hatua ya 12: Kuandika Mchanganuo wa Biashara (Business Plan)
• Baada ya kufanya hayo yote sasa ni wakati mzuri wa kuandika mchanganuo wa biashara yako
• Mchanganuo wa biashara ni maelezo ya kina ambayo inaonyesha biashara yako ilikotoka, inakokwenda, hali ya masoko, sekta, kifedha na uongozi wa biahara yako. Ni taarifa muhimu ya kuwavutia wawekezaji na watoa mikopo kama mabenki
Mambo muhimu ya kujua katika kuandika Mchanganuo wa Biashara
1. Kasha la nje
2. Maelezo wa biashara yako
3. Historia na maelezo ya biashara yako
4. Maelezo ya bidhaa au huduma ya biashara yako
5. Mchanganuo wa masoko
• Washiriki, uwezo an madhaifu yao
• Ukubwa wa soko
• Mgawanyo wa soko
• Aina ya soko/masoko
6. Mkakati wa utekelezaji
• Uongozi na usimamizi wa kazi
• Uchambuzi wa madhaifu, nguvu, fursa na hatari zinazokabili biashara yako
• Mkakati wa Uzalishaji
• Mkakati wa kuuza
7. Mpango wa fedha
• Uchambuzi wa mahitaji ya mtaji
• Wapi utatoa mtaji
• Matumizi ya mtaji
• Makisio ya Mauzo
• Uchambuzi wa kurudisha gharama (break even analysis)
• Makisio ya faida au hasara
• Makisio ya mzunguko wa fedha katika biashara yako (cashflow)
• Makisio ya oanisho la mali na madeni ya biashara yako (balance sheet)
• Ulinganifu wa sehemu mbalimbali za biashara (business ratios)
8. Viambatanisho
1. Lesseni
2. Cheti cha ulipaji kodi
3. TIN
4. Cheti cha usajili
5. Mikataba
6. Risiti za manunuzi hasa mali za Biashara
7. Taarifa zingine ambazo hazikupata nafasi ndani ya mchanganuo huu
8. Taarifa zingine zinazoweza kuifanya biashara au kampuni kuaminika zaidi
Hatua ya 13: Kupanga juu ya pesa.
Kutafuta mikopo kwa kufuata utaratibu wa taasisi za fedha husika
Taasisi nyingi huhitaji yafuatayo
1. Dhamana ya mkopo
2. Uzoefu wa biashara husika
3. Mchanganuo wa biashara
4. Maombi ya mkopo
Hatua ya 14: Ufahamu wa kiufundi.
Hii ifanywe ili mwenye biashara apate ufahamu wa kiufundi juu ya biashara yake hasa kutoka kwa taasisi husika au mshauri wa biashara (consultant).
Hatua ya 15: Kujua vyanzo vya nishati:
Kama ni umeme hakikisha iko sawa na umeme utakidhi matakwa ya biashara.
Kama ni mafuta uhakikishe mafuta inapatikana na bei haitaadhiri bei ya bidhaa
Hatua ya 16: Kuweka vifaa: (Machines installation)
Wataalam husika wafanye hii kazi
Hatua ya 17: Kuajiri wafanyakazi.
Wafanyakazi wako wengi mtaani, lakini kumpata mtu atakayekidhi matakwa ya biashara yako kwa maana ya ubora na kufikia lengo la uzalishaji inahitaji usambazaji wa taarifa kwa upana zaidi na kwa maeneo maalum ambayo unategemea wafanyakazi watoke. Mfano vyuoni, makanisani nk
Unashauriwa pia kutumia marafiki na ndugu wa karibu ili upate mfanyakazi ambaye ni bora zaidi
Hatua ya 18: Kujua upatikanaji wa malighafi/biadha/huduma
Kama unazalisha malighafi bila ubishi ni kiungo muhimu kwa biashara yeyote inayohusisha kuzalisha bidhaa. Vivyo hivyo kama unachuuza, sehemu ya kupata bidhaa kwa bei ya jumla ni muhimu uzijue na kuziweka kwenye database yako. Na pia kama wewe ni mto huduma, unatakiwa kujua utapata wapi huduma zitakazokuwezesha wewe kuwahudumia wateja wako vizuri. Vyanzo vya kupata malighafi/bidhaa/huduma ni muhimu ijulikane na iwe ya uhakika.
Hatua ya 19: Uzalishaji mali
• Uzalishaji wa majaribio , Kuuza kwa majaribio kutoa huduma kwa majaribio muda – miezi 2-6, nk
• Kuanza biashara rasmi
• Kutunza siri ya unavyozalisha au kutoa huduma tofauti na wengine
• Tunza vizuri siri zingine za biashara yako
Hatua ya 20: Kuhakikisha bidhaa yako hainakiliki
• Kama unatengeneza biadhaa hakikisha fomula na mbinu ulizotumia ni ngumu na zimefanywa siri kubwa
• Pia hakikisha unalinda hati miliki ya huduma au bidhaa husika katika ngazi husika za usajili na utambuzi
Hatua ya 21: Usalama wa biashara yako
Epuka majengo ambayo ni rahisi kuwaka moto, kubomolewa na wezi, wizi katika pesa za mauzo, utapeli wa bidhaa katika kununua na kuuza nk.
Hatua ya 22: Kuuza (Selling)
Kufikia wateja (fikiria utamfikiaje mteja wako wa kwanza – maelezo zaidi yatakuwepo katika mchanganuo wa biashara)
• Kusambasa huduma/bidhaa
• Kuweka bei
• Kutangazia biashara
• Promosheni nk.
Hatua ya 23: Utafiti wa soko (Market Research)
• Hii ifanywe kila mara ili kujua kama wateja wamebadilika au bado Ili kujua kama wanapenda huduma/bidhaa zako au la.
• Kujua biashara yako imekamata asilimia gani katika soko
• Kupata maoni ya wateja ili kuboresha biashara/huduma/bidhaa
Namna ya kufanya utafiti
Utafiti wa kuendelea
Kila mteja anaponunua bidhaa, ajaze fomu maalum ya maoni. Mfano ya jinsi alivyohudumiwa, bei ya bidhaa, usindikaji, ubora nk
Utafiti maalum
Huu ufanywe wakati wa kutoa vivutiuo maalum au promosheni maalum.
Mteja wa promosheni ajaze fomu maalum ya maoni. Mfano ya jinsi alivyohudumiwa, bei ya bidhaa, usindikaji, ubora nk
Hatua ya 24: Kusimamia na kuthibiti biashara
Hii ni kuhakikisha kuwa biashara inakwenda kama ilivyobuniwa /pangwa. weka mifumo ya kudhibiti na kuhakikisha ubora unafikiwa nk
Hatua ya 25: Kutathmini biashara
Hii ni kujua kama biashara imekwenda kama ilivyobuniwa /pangwa.
Mambo ya kuangalia
1. Mapato na matumizi
2. Bajeti iliyopita
3. Matokeo ya utaifit/wa soko
Hatua ya 26: Kufanya maboresho/mabadiliko
Unaweza kumuajiri au kumtumia mtaalam wa sekta hiyo kufanya taadhmini ya biashara yako.
Fanya sawa sawa na matokeo ya tathmini/utafiti
Saturday, August 5, 2017
Subscribe to:
Posts (Atom)