Thursday, July 14, 2016

RIWAYA YA KICHWAMAJI



MUKHTASARI NA UCHAMBUZI WA FASIHI: RIWAYA YA KICHWAMAJI.
        UTANGULIZI:
Kichwamaji ni riwaya ya kisasa, ambayo imejikita zaidi katika nadharia ya “utamaushi (udhanaishi)” katika kuangalia maisha ya sasa.Ni riwaya ambayo inasadifu maisha ya waafrika wa dunia ya leo, zaidi ikizungumzia na kuweka bayana mambo au mataitizo ambayo waafrika wa sasa wanakumbana nayo; zaidi ni waafrika wa mashariki mwa bara. Riwaya hii, kwa kina imeweka wazi maudhui yake, ikijikita sana katika kuchora mandhari ya Afrika ya Mashariki-Tanzania katika wilaya ya Ukerewe. Kutokana na nadharia iliyofuatwa kuandika riwaya hii, zaidi matatizo ndio yanaonekana kikwazo hasa kwenye mafanikio ya mwanadamu hadi msanii kufikia hatua ya kuona kwamba maisha hayana umuhimu wowote. Vilevile na kumchukulia Mungu kuwa hayupo. Mwandishi anatanabaisha kuwa binadamu mwisho wake, ni kifo. Dunia anamoishi binadamu imejaa matatizo, vikwazo vya kila aina: kwamba maisha ni vurugu, maangaiko na misukosuko n.k. Wahusika wa riwaya hii, wamechorwa kuwa ni watu wanaoangaika kutafuta maana ya maisha, kupata fasili  ya maisha ni nini? Hivyo tunaona namna ambavyo wahusika wakuu katika simulizi ya riwaya hii; wanapitia katika shida na maangaiko mengi. Hawafurahii uwepo wao wa maisha.
Vilevile msuko wa visa na matukio katika riwaya hii, ni wa kuonesha jinsi gani mwanadamu katika kuishi anapata taabu sana. Pengine hata mafanikio wanayopata hawayafurahii kwa muda mrefu: ni furaha ya muda mfupi. Mazingira na muktadha wa riwaya hii, yamejengwa kwa hali ya chini: hasa zaidi katika hali ya umasikini, ambapo mara nyingi huwa ni maisha ya kuangaika na kutoa jasho nyingi ili kuweza kupata mafanikio.

MAUDHUI YALIYOLENGWA KATIKA RIWAYA HII:
Katika riwaya hii mwandishi ameweka hadharani maudhui yake: kwa kuonesha wazi matatizo/vikwazo/misukosuko inayomkatisha tamaa mwanadamu katika maisha yake. Miongoni mwa matatizo aliyoyabainisha mwandishi, ni kama: kifo, njaa, ugomvi, dharau, kulipiza visasi, umasikini, uwepo kwa matabaka ya walio nacho na wasionacho, kukatika kwa furaha ya mtu ghafla, dhuluma na wivu,kunyanyasika kwa masikini kunako sababishwa na matajiri pia viongozi kuwadharau na kuwakomoa raia wa kawaida wasio na ofisi za kuajiriwa na serikali. Haya yote ni baadhi ya vikwazo anavyokumbana navyo binadamu anayetafuta furaha ya maisha na mwishowe anaishia kuvikosa kabisa; ama kuvipata lakini kwa muda. Mtazamo na mwono huu unamfanya mwandishi wa riwaya hii, aone kwamba mwanadamu ameumbiwa matatizo tu, katika maisha yake na kupata raha yeye kwake ni nadra sana. Hivyo kwake yeye anatazama maisha kama mtihani na adhabu kubwa aliyopewa binadamu: kwani hawezi kuwa na unafuu juu ya maisha.
Mtazamo huu pia unampa picha msanii wa riwaya hii kuwa na maswali mengi juu ya uwepo wa Mungu. Na kusema kuwa Mungu hayupo na kama yupo kwanini watu wanateseka namna hii?, au kwa nini Mungu anakuwa na ukatili namna hii?, kama tunavyosoma na kouna (uk.51) msanii anasema; …niliposema hivyo tu wazee hawakuwa na shuku ya kuniuliza tena maswali. Hawakuona tofauti kubwa kati yangu na wao. Mambo yaliharibika nilpoanza kuwaambia kwamba huenda hakuna Mungu….vilevile katika (uk.124) mwandishi anashikilia mawazo yake ya kuwa hakuna Mungu: mstari wa pili wa ukurasa na kuendelea, msanii anasema;
 “Unafikiri nini juu ya watu wasioamini kuwa Mungu yupo?”
“Ni wajinga,” Manase alisema mara moja.
“Hivi wewe unafikiri mtu asiyeamini Mungu ni mtu gani?” nilimwuliza.
“Ni mtu ambaye anataka kumfahamu Mungu kwa kutumia kichwa chake. Mungu hawezi kueleweka kwa akili.”
“Hapo ndipo sikubaliani nawe. Mtu asiyeamini Mungu ni mtu asiyeamua kuwako kwa Mungu kwa kutumia milango ya fahamu peke yake. Licha ya milango ya fahamu mtu asiyeamini Mungu anatumia akili zake.”
“Unaona, Manase; mwanadamu ameamua kwamba kuna Mungu kwa sababu ya hali yake ya woga iletwayo na milago ya fahamu. Kwahiyo mtu anayeamini kwamba Mungu yupo ni yule aamuaye kwa kufuata milango ya fahamu yake. Kwake fahamu zinatawala bongo.”
Pia mwandishi anazidi kukata tamaa zaidi na kufuata msimamo wa kuwa na mtazamo hasi juu ya uwezo na uwepo wa Mungu: hasa pale anapomchora mhusika Kazimoto baada ya kufiwa na mtoto wake mchanga, aliyekuwa akimtegemea sana na mke wake lakini mtoto huyo alikufa muda mfupi baada ya kuzaliwa. Haya ni maneno ya Kazimoto: “…usiku nikiwa na mke wangu, mawazo mengi yalinijia kichwani. Nilianza tena kufikiri juu ya Mungu.Kama kweli Mungu alikuwepo sikuona  kwanini aliweza kufanya ukatili mkubwa kama huo. Matumaini yetu yote; kazi na taabu tuliyopata-yote hayo chini! Sikuona maana ya maisha….” (uk.180).
              Mtazamo huu wa mwanafasihi E.Kezilahabi, umezidi kuteka mawazo yake katika riwaya hii. Ni wazi kuwa kwake yeye haoni umuhimu wa maisha, pia amani ya mwandamu hapa duniani ni ndogo. Maswali mengi yameteka riwaya hii: kama, maisha ni nini? Au maisha yana maana gani? Mwanadamu ni kiumbe wa maisha gani na umuhumu wa kuishi uko wapi/ni upi kwake? Ni kwa nini furaha haidumu katika maisha ya binadamu? Mwisho wa maisha ya mwanadamu ni upi au ni nini?  Kifo ni nini na kwa nini watu wanakufa? Ni kwa vipi maisha yawe mafupi lakini yenye vikwazo mbalimbali? Mkondo wa riwaya ya “Kichwamaji”,ni wa kidhanaishi, kwa sababu mwandishi amejikita zaidi kuonesha maisha ya binadamu yalivyoumbwa kwenye bahari yenye kila machafuko ya mawimbi mazito; hadi mwishowe, tunaona mhusika mkuu Kazimoto akikata tamaa ya kuishi hadi hatua ya kujiua kwa kujilipua kwa bunduki(bastola).
         Ni dhahiri kuwa, maswali haya yanamfanya mwandishi, ashindwe kupata mwafaka wa maisha yake. Pia majibu ya maswali haya yanakosekana; pengine yakionekana ni majibu yenye mafupi yasiyoweza kupata ufumbuzi wa maswali haya kwa kina. Katika kuendelea kuichambua kwa kina riwaya hii, tutaona kwamba mbali ya kuwa riwaya hii imejengwa katika nadharia ya udhanaishi, inatoa na kubainisha wazi matatizo yanayoikumba jamii ya sasa ya mtanzania. Tutaingia kuitazama na kuielewa kwa undani zaidi riwaya hii kwa kuzama katika kila sura ya kitabu hiki.


SURA YA 1
Katika sura hii msanii anaanza kwa kutuonyesha bughudha, maangaiko, taabu na karaha anazo kumbanazo mtu katika kutafuta huduma kwenye jamii anamoishi. Msanii anadhihirisha mambo haya, kwa kutumia kalamu yake akimwaga wino( uk.1)…watu tulikuwa tukingoja kuingia ndani ya ofisi ya Mkuu wa Wilaya tulikuwa wengi. Wazee kwa vijana, wanawake kwa wanaume. Wote kama wagonjwa wangojeao kumwona daktari,…anaendelea kusema katika mstari unaofuata …mmoja alipokuwa akiingia ndani tuilkuwa tukisukumana kwa matako ili kuziba nafasi…Lakini msichana aliyekuwa amekaa karibu nami mkono wa kushoto haukuonekana kuwa na raha: alikuwa amekaa karibu na mzee na wakati wote msichana huyu alikuwa ameweka kitambaa juu ya pua yake…
Maneno haya yana uzito mkubwa kwa kuyatafakari katika mkondo wa riwaya hii, ama tunaona watu wengi ambavyo wanaangaika kupanga mistari ili kuweza kuhudumiwa katika taasisi. Ni utaratibu ambao unawafanya watu wengi waumie kwa kuchelewa na kuharibu ratiba nyingine. Inaonekana dada katika ule mstari hana raha na ameweka mkono wake puani. Na tunaambiwa chanzo ni kukaa karibu na mzee mmoja. Vile vile msanii anaonesha kuwa maisha hayana maana, tunaposimuliwa kuwa: msichana ambaye mhusika mkuu yaani kazimoto, anamwona mzuri na mwenye umbo zuri, mwenye kuvutia: ila anatolewa kasoro na wasichana waliokuwa wamekaa karibu naye (uk.1-2)
“Mwishowe yule aliyekuwa ametukawiza alitoka nje hali akitabasamu. Alikuwa msichana maji ya kunde, mrefu na mwenye uso wa mviringo. Ilikuwa alipoanza kutembea nilipotambua kwamba kiuno alichokuwa nacho kiliweza kuvutia macho ya watu na kuleta ugomvi. Alisita kutabasamu mara tu alipoona kwamba macho yote yalikuwa yakimtazama, na aliposikia watu wakiguna alitembea mara moja kuelekea mlangoni ili atoke upesi. Nilisikia wasichana waliokuwa wamekaa karibu nami wakimtoa makosa:
“Ee, dada! Poda kuzidisha!”
“Viatu vitembeze vizuri!”
“Hata mkoba wenyewe hajui kuushika!
Anaupakata kama mtoto!”
“Hata kitambaa hawezi kukifunga!”
Katika maisha kuna kutafuta na kukaosa. Hili ni jambo ambalo huwakumba watu wengi ambao hutafuta riziki kwa ajili ya kujipatia kipato. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa kijana Kazimoto: msomi ambaye aliamua kujishughulisha na kufanya kazi mbalimbali ili ajipatie chochote muda wa likizo. Alienda kuomba kazi kwa mkuu wa wilaya, ambaye walikuwa wakisoma pamoja shule ya msingi.Lakini alikosa fursa hiyo baada ya kutoelewana na mkuu wa wilaya kwa sababu za ujana wao zilizohusu wivu wa wasichana. Jambo ambalo lilimfanya Kazimoto kuona uchungu wa maisha; vilevile kutaka kulipiza kisasi alichofanyiwa na rafiki yake huyo wa zamani wakati wanasoma shule ya msingi. Mkuu huyo wa wilaya aliyeitwa Manase aliharibu ndoto za kusoma za Rukia ambaye ni dada yake Kazimoto. Kutokana na uchungu wa kuona dada yake anaacha shule kwa sababu ya Manase: na yeye ana kazi nzuri alafu amemnyima kazi ya muda Kazimoto, ndipo Kazimoto anakata shauri ya kulipiza kisasi kwa Manase.


SURA YA 2
Katika sura hii tunaona mkondo wa udhanaishi unaendelea. Katika masimulizi; Kazimoto bado ana hasira ya kuendelea kulipiza kisasi kwa Manase kutokana na kumharibia masomo dada yake. Ni sura ambayo msimulizi anazidi kutusasambulia kisa kizima ambacho kinamfanya Kazimoto afikirie sana juu ya maisha ya dada yake yalivyoharibiwa na rafiki yake wa karibu Manase. Rukia alishindwa kuendelea na darasa la tisa: lakini Kazimoto alikuwa na shauku ya kuendelea kumsomesha ili apate elimu bora.(uk.18)…Rukia alishindwa kuingia darasa la tisa, lakini mimi nilikuwa na nia ya kumwelimisha…
Kazimoto alifanya juu chini na kumtafutia mdogo wake shule, alifanikiwa kuipata Dar es Salaam. Kama asemavyo msimulizi katika (uk.18) …nilimtafutia shule na baada ya kuipata kichini chini kama ilivyo kuwa kawaida, nilipata shule moja huko Dar es Salaam… Aliamua ampeleke Dar es Salaam mdogo wake ili akaendelee na masomo ila shule haikuwa na mabweni: Manase alikata shauri ya kuomba Manase akae na Rukia kwani Kazimoto alikuwa bado anasoma chuo kikuu Dar es Salaam na hakuwa na ndugu ye yote huko wa kukaa na dada yake Rukia. Aliona rafiki yake Manase ndiye ambaye angeweza kukaa na Rukia kipindi anaposoma.
 “Tabu sasa ikawa ni mahali pa kupanga: shule yenyewe haikuwa na malazi kwa wanafunzi. Manase wakati huo alikuwa akiishi Oystebay, na kwa kuwa alikuwa na nyumba kubwa nilifikiri ataweza kuishi na ndugu yangu. Licha ya nyumba kuwa kubwa wakati huo uliuwa ni wakati ambao uhusiano kati yangu naye uilikwa mzuri.Nilipomwambia Manase taabu yangu alikubali kukaa na ndugu yangu. Wakati huo mimi nilikuwa nimekwisha ingia chuo kikuu.”
Baada ya Manase kuamua kukaa na Rukia, mambo yalienda kinyume na matarajio. Ndipo msanii anatanabaisha jinsi ambavyo Manase alimgeuka na kumuharibia masomo Rukia kwa kufanya naye mapenzi ya lazima alipokataa wakati akijua kuwa ni ndugu yake wa jirani na pia ni mwanafunzi. Rukia alipata mimba na kufukuzwa shule na baadaye kufukuzwa na Manase nyumbani kwake. Rukia alirudi kijijini akiwa mjamzito aliyeenda kusoma na kurudi nyumbani akiwa amechuma tunda la mimba. Kazimoto anasema kuwa baada ya Manase kuanza ukatili huo Rukia alimwandikia barua za kumjulisha juu ya hali ile: ili ikiwezekana ahame kwa Manase lakini kutokana na uwezo mdogo wa kiuchumi, Kazimoto alimsihii aendelee kuvumilia: lakini hali ilikuwa ndivyo sivyo kwa dada yake hadi kumwandikia barua kuwa: “Kaka usiponitafutia mahali pengine pa kukaa mimi nitarudi nyumbani. Heri kuacha shule!” Hali hii iliendelea kumkumba Rukia hadi alipotimuliwa na Manase kwa matusi juu yake akimwita Malaya. Msimulizi anatuonesha kwa maneno ya Kazimoto kuwa baada ya muda mfupi kumsihi dada yake aendelee kuvumilia: alipokea barua kutoka kwa Rukia ikisema kama ifuatavyo:
Barua yenyewe: (uk.19)
Kaka mpendwa,
     Moyo wangu siku hizi hauna raha. Lakini leo nimechukua kalamu ili nikueleze mambo yote. Nimeona kwamba siwezi kuwa nakuficha wewe mambo, hali mambo yenyewe hayawezi kufichika. Wewe ukiwa kaka yangu na ndiye uliyenitafutia nafasi hii ya shule ninakupa heshima. Fahamu kwamba mambo haya sijapata kumweleza mtu mwingine isipokuwa wewe peke yako.
          Kaka, uliponileta hapa nilikaa kwa raha kwa muda wa juma moja tu. Baada ya juma hilo, niliona Manase anaanza kunitazama kwa njia ya ajabu. Baada ya majuma mawili mambo yalizidi kuwa mabaya, kwani nilipokuwa naoga niliona jicho lake kwenye tudu la ufunguo.
          Mwishowe aliniambia wazi alichokuwa anataka. Nilimwambia: Manase! Kaka yangu akifahamu litakuwa jambo la aibu sana! Lakini yeye alijibu kwamba wewe ni mwanaume kama yeye. Alifikia hata hatua ya kutumia nguvu! Na kweli alitumia nguvu bila utashi wangu.
        Kaka, sitaki kukupotezea muda wako wa kujifunza kwa kusoma barua ndefu. Mimi maisha yangu yameharibika. Shule nimekwisha acha. Jambo ambalo limenisikitisha sana ni hili lifuatalo: Jana usiku Manase alirejea nyumbani mlevi. Alikuwa na tikiti ya basi. Baada ya kunitukana kwa maneno ambayo siwezi kukuandikia, alianza kupanga vitu vyangu sandukuni. Leo atanisindikiza hadi kituo cha basi. Kaka, machozi yanilengalenga, sijui nitasema nini kwa baba na mama. Usifike kuja kuniaga kwenye kituo cha basi nisije nikazimia.
            Sina mengi.
                                                  Nduguyo,
                                                                                     Rukia Mafuru.

 Barua hii inadhihirisha udhanaishi kwa msanii wa riwaya hii. Kwani katika barua anatuonesha namna mtu ambavyo anahangaika kujikomboa katika hali ngumu ya maisha: lakini mambo yanaenda kinyume na kugonga mwamba na shida kuzirudia. Katika sura hii mwandishi anaenda mbali zaidi, akisimulia namna ambavyo Kazimoto anapoenda likizo anafika njiani na kukutana na watu wakimuuliza, na wengine kumshangaa kurudi kwao kutokana na shida pamoja na mambo ya ajabu yaliyo kuwa yakitokea kwao Kazimoto. Kijiji kizima kilikuwa kikifahamu mambo hayo na ndio maana kila mtu aliyekutana na Kazimoto njiani alimshutuka na kumshangaa. Mfano, Kazimoto anasema: …mtu wa kwanza kuzungumza naye alikuwa kijana mmoja tuliyekuwa tukisoma pamoja zamani. Yeye sasa alikuwa ameoa na alikuwa na watoto watatu.
         “Wewe kwa nini umekuja nyumbani?” aliniuliza kwa mshangao bila hata kunisalimu kwanza.
“Kwa nini? Mbona huwa nakuja nyumbani karibu kila likizo?”
“Heri ungebaki huko. Huku umejileta hatarini.”
“ Hatari gani?”
“ Hatari gani? Hujui?”
“Hata sina habari!”
“Ndugu yangu,utasimuliwa nyumbani.”
Mtu wa pili kukutana naye alikuwa mzee. Mzee huyu alikuwa akipeleka ng’ombe wake mtoni kunywa maji. Alikuwa ameenea vumbi nyweleni.
“Kazimoto! Umekuja kujionea mwenyewe!” alisema.
“Kuona nini?”
“Ha! Huna haraka?”
“Hata sina!”    
“Mambo Fulani yametokea pale nyumbani kwenu ambayo yameshangaza kijiji cha Mahande.”
Kazimoto aliendelea kuelekea nyumbani kwa wasiwasi, huku kila mtu aliyekuwa anakutana naye njiani alizidi kumtia wasiwasi na kumuuliza juu ya matatizo ya nyumbani kwao. Katika (uk.23), tunaona Kazimoto anakutana na Mzee Kabenga: na kumuuliza habari za nyumbani kwao, ambapo mzee Kabenga anashindwa kumsimulia yaliyokuwa yakitokea kwa jirani yao; anamsihi Kazimoto aende nyubani na ataweza kujua habari zote huko nyumbani kwao. Msimulizi anazidi kusimulia matatizo yaliyokuwa yakiikumba familia ya kwao Kazimoto: mataizo hayo yaliweza kubainika kuwa ni imani za kishirikina. Ni watu ambao walikuwa wakiisumbua familia ya mzee Mfuru kwa sababu ya kutaka kuchukua shamba lao. Mambo haya yanaongelewa katika sura hii kuanzia (uk.23-39).Ni matatizo na dhoruba ambazo walikuwa wakikumbana nazo familya ya mzee Mfuru, hasa wakati wa usiku na kuwanyima usingizi: hakika walikosa amani na kukata tama ya kuishi hadi kufikia hatua ya kumwambia Kazimoto kuwa wanaangaishwa na wachawi, kwa kuwa yeye amesoma hadi chuo kikuu; hivyo atafanikiwa.  Mama yake Kazimoto anamwambia mtomto wake hivi: … “Hufahamu kwamba sisi wote hapa maisha yetu yote yamo hatarini? Kwa kuwa wewe umesoma nafikiri we ndiwe utakuwa wa kwanza kuuawa.”(uk.24).



SURA YA 3.
Mkondo au nadharia ile ile ya udhanaishi bado ndio mwongozo wa kitabu hiki. Katika sura hii mwandishi anatueleza jinsi ambavyo: mhusika Kazimoto, anavyoamka asubuhi na mapema bila kuwaaga watu aliokuwa akiishi nao na kwenda kumuona na kumpa pole rafiki yake Kamata anayeishi kijiji cha Saku, kwa matatizo yaliyomkumba. Kazimoto alifika kwa rafiki yake Kamata mnamo saa nne asubuhi na kumkuta mke wake Kamata, jina lake ni Matilda. Katika riwaya hii, tunambiwa kuwa Kamata hakuwepo na alikuwa kazini kwake; alikuwa ziwani kwani shughuli yake kubwa ilikuwa ni uvuvi. Kazimoto alienda kumpa pole rafiki yake kwa matatizo yaliyomkuta. Kamata anamsimulia matatizo hayo:
“Kazimoto, furahi kuniona sasa. Nilikuwa maiti, na ninafikiri kwamba sasa ungekuwa unalia karibu na kaburi langu. Nilikuwa mfu. Hadithi yenyewe ni hivi: siku moja vijana wawili walinipitia hapa kwenda kunywa pombe. Vijana hao ni majirani. Tulipofika huko kwenye pombe tulikunywa sana. Kumbe wenzangu walikuwa na nia mbaya. Giza lilipoingia walikuwa wanajitia pombe kidogo, mimi nikitiliwa pombe nyingi. Mwishowe nilijiona naanza kulewa. Niliwaomba ruhusa kuondoka, lakini wao walikataa. Waliahidi kunisindikiza mpaka nyumbani. Niliendelea kunywa karibu kama saa sita za usiku waliniambia kwamba walikuwa tayari kunisindikiza. Nilijaribu kusimama, nilijiona bado na nguvu za kuweza kutembea bila kushikwa. Tulipofika mbali kutoka mahari pa kunywea pombe, mmoja wao alisema: “Kamata.”
“Nilisimama. Mara niliona kila mmoja wao ameshika rungu. Hofu ilinishika na pombe yote  iliruka. Niliona mwisho wa maisha yangu hapa duniani.
“Jamani! Kweli  mniue! Mniue kabisa,” nilijitetea.
“Ua kabla hajasema maneno mengi!” mmoja alisema. Hapo hapo nilipigwa rungu la mgongo. Nilianguka chini.
“Jamani kweli sasa mmeniua!”
“Mara moja nilisikia rungu linalia juu ya kichwa change. Nilizimia.
Kesho yake asubuhi nilipozinduka nilijiona nimelala ndani ya maji. Majani yalikuwa marefu hata sikuweza kuona  mahali popote. Akili ziliponirudia sawa sawa nilikaa kwa muda nilifikiri.. nilikumbuka hadithi kidogo. Niliona nguo zangu zimeenea damu. Nilipojishika kichwani nilishangaa kutupa kidole ndani ya shimo. Nilianza tena kuogopa. Njljiona maii tena. Nilijaribu kusimama. Maumivu yalikuwa mengi mno. Niliposimama nilijiona kwamba nilikuwa nimelala karibu na ziwa. Nilisikia sauti za watu. Nilijivuta polepole. Wale watu waliponiona walistuka, kama kwamba waliona mzuka fulani. Ndio wale vijana ambao ulikuwa nao ziwani. Nilipowakaribia  walinitambua: “Kamata! Umekuwaje?”waliniuiza. nipelekani nyumbani nikamwone mke wangu,” niliwaambia. “Waliponifikisha nyumbani, mke wangu alianza kulia baada ya kunitafutia maji na kunisafisha. Wale vijana waliosha vidonda vyangu. Maumivu yalikuwa makali. Niliomba nipelekwe hospitali ya Bukonyo…”(uk.44-45).
Matatizo yaliyomkumba Kamata, ni matatizo ambayo tumekuwa tukisikia yakiwakumba watu, na hata pia kushuhudia yakiwakumba ndugu zetu. Kazimoto alitaka kujua chanzo cha hayo yote: Kamata alimweleza kama ifuatavyo:
“Sikutaka kukueleza pale nyumbani kisa kilichofanya nipigwe.”
“Ebu nuileze.”  “…sababu yenyewe ni kwamba wale vijana walijaribu kumtongoza mke wangu. Alipowakataa waliona kwamba alikuwa akiwakataa kwa sababu mimi nilikuwa hai. Kwa hiyo walikata shauri ya kuniua…(uk.47). Vile vile masimulizi katika sura hii yanazidi kuhusu maisha yenye raha kidogo pamoja na shida. Ndipo tunapomuona Kazimoto anakutana na mwanamke Nyabuo wa kufanya naye mapenzi ya muda pale walipokutana kwenye pombe alipokuwa kwa Kamata. (Uk.52-60). Pia tunaona kwenye sura hii ndipo Kazimoto, anapowaambia wazee waliokuwa wakimuuliza maswali ya kuhusu kisomo: kuwa hakuna Mungu.( Uk.51). Kazimoto anasimulia jinsi ambavyo alipata misukosuko njiani wakati alipokuwa anarudi nyumbani kwako, alipata ajali njiani. (Uk.62-63)
“Nikiwa juu ya baiskeli nilijiona katika hali ya upweke. Mawazo mengi yalinijia kichwani. Mara niliona baiskeli yangu inaongezeka mwendo: nilikuwa nimefikia mwendo mkali. Nilijaribu kufunga breki baada ya kuona kundi la ng’ombe mbele yangu barabarani kabisa. Nilifunga breki kwa nguvu. Nilisikia kitu fulani kama mlio wa chuma. Baada ya kupunguza mwendo baiskeli ilianza kwenda kasi sana. Nilitambua mara moja kwamba sikuwa na breki za nyuma. Niliogopa kutumia za mbele. Kutahamaki niliona ng’ombe mmoja hatua kumi hivi mbele yangu. Nilimgonga ubavuni. Nilisikia ng’ombe analia. Baiskeli ilianguka mbali na mimi nilipita juu ya mgongo wa ng’ombe na kuanguka upande mwingine. Kidogo yule ng’ombe anikanyage tumboni aliporuka kuwakimbilia wenzake. Nilisikia watoto waliokuwa wakichunga wale ng’ombe wakinicheka na kunizomea.
Hilo! Linabahati! Kama lingeanguka juu ya pembe, leo lingeona cha mtema kuni!”
“Tazama mandizi yake!” walisema.
Hii ni safari ya kumuona rafiki yake ambayo misukosuko ya maisha ilimkumba mhusika mkuu Kazimoto wakati akienda na kurudi kutoka kumsabahi rafiki yake Kamata.

SURA YA 4
Hiii ni sura fupi ambayo inaeleza jinsi Kazimoto alivyofika nyumbani kwao usiku akitoka kwa Kamata. Aliwasili nyumbani kwao usiku na kukuta ndugu zake wamekwisha lala; lakini mibweko ya mbwa waliokuwa wamewafuga ndio iliyomfanya mama yake ashtuke na kwenda kuangalia chumbani kwa Kazimoto na kumkuta amewasili toka safarini: baada ya kondoka bila kuaga nyumbani. Mama yake alichukua jukumu la kumhoji kama mzazi ili kujua alipokuwa, kwa muda wote huo (uk.64). Kazimoto hakupendezwa na maswali aliyokuwa akiulizwa na mama yake, kwani yalimuudhi na kutopenda kabisa kusikia akiulizwa hivyo.
Baada ya hapo kesho yake, mama yake alichukua jukumu la kumtibu mtoto wake: kwa kumkanda sehemu alizoumia alipopata ajali, na baadaye baba yake Kazimoto na Kabenga walimwita Kazimoto na kumpeleka kwenye chumba cha maongezi ili kumuonya mtoto wao kwa kuondoka bila kuaga mtu hali akijua kuwa aliwaacha watu humo ndani.(uk.66-67).


SURA YA 5
Sura hii tunapata kujua kwa ufupi kuhusu wahusika Vumilia na Tegemea(uk.68): ambao maisha yao yalikuwa ni ya taabu. Vumilia na mama yake Tegemea waliishi sana maisha ya kuwa na wanaume wengi bila kuolewa kwa muda mrefu kidogo. Ni sura ambayo tabia za Kazimoto za kuingia kimahusianao na msicha Vumilia zinapoelezwa. “Mimi nilimfahamu Vumilia ambaye nilikuwa na uhusino naye. Ya zamani hayanuki.”(uk.69). Kazimoto anaamua kumfuata usiku Vumilia akiwa na mdogo wake Kalia: ni baada ya wazazi wake kuwa wamesinzia kutojua kinachoendelea. Wanafika kwa Tegemea na kumchukua Vumilia usiku. Baada ya kufika kwa Tegemea muda huo ambao hapakuwepo na kulandalanda kwa watu kwa kuwa ulikuwa muda wa watu kupumzika: Kazimoto na Kalia walishtuka na kushangaa kusikia sauti ya Kabenga ndani ya chumba cha Tegemea. Alikuwa akicheka na kunong’ona na Tegemea ndani ya chumba cha kulala. Mara walikuwa wakizozana na kupatana juu ya mambo yao ya kimapenzi humo chumbani, na vijana hawa wawili waliokuwa wakiwanyemelea katika dirisha la chumba cha Vumilia waliwasikia.
        …Kalia alikuwa akicheka kwa ndani hali ameziba mdomo…”
“Anayezungumza humo ndani umemtambua?”aliniuliza.
Nafikiri nimemtambua.” Ni Kabenga.”
“Kumbe mzee huyu ni hatari! Uhusiano ulianza lini?”
“Tangu zamani,”Kalia alisema, “isipokuwa mlikuwa bado hamjagongana. Kama nasikia huu ndo umeleta mpango wa kumuoza Vumilia kwa Manase. Tuza anapinga sana uchumba huu na Manase mwenyewe hapendi. Juzi juzi walimtuma Vumilia kwenda kuzungumza kidogo na Manase. Lakini nasikia Vumilia alimkuta Manase anaishi na kimada. “Gonga dirisha umchukue mke wako, twende naona baridi. (”uk.70-71)

Vilevile , kuna msemo usemao kuwa, tabia urithishwa. Hili ndilo lililomkuta Kalia na Kaka yake baada ya Kalia kuona sasa naye kusindikiza kaka yake katika safari za kuchukua vimada, wakati yeye anaambulia patupu ilikuwa imefika kikomo. Naye sasa alidai kuwa anataka kuwa anapata wasichana pindi kaka yake naye anapopata. Kazimoto anasema kuwa; ndani ya nyumba Kalia alianza kutoa manung’uniko yake ambayo nilifikiri kuwa ya kitoto.
“Bwana , nimeona sasa siwezi kuwa nakupeleka kuchukua wanawake. Wewe unapata mimi siambulii lolote. Usiku kama wa leo siwezi kupata usingizi vizuri.” Vumilia alicheka.
“ Sasa unataka tugawane?” nilimwuliza. “Nataka na wewe uwe unanisaidia kupata wasichana. Yaani siku unayoleta name niwe naleta.(”UK.72)’
Si hayo tu, bali pia, katika sura hii ya tano ndipo pia mihimili ya udhanaishi inapojidhihirisha wazi kwetu: tunaposoma riwaya hii kwa umakini. Mawazo na ndoto za kuwepo maisha baada ya kifo ndipo tunapokutana nayo tena katika mazungumzo kati ya Kazimoto na Kalia. (Uk.73-74) … Asubuhi na mapema Kalia alikuja chumbani mwangu.
“Amekwenda?”
“Nilimsindikiza peke yangu. Wewe ulikataa!”
“ Mimi sikukataa isipokuwa name sasa anahitaji mwanamke.”
Alinyamaza kwa muda. “Leo nimeota ndoto ya ajabu,” alisema tena.
“ Ulikuwa na mwanamke?”
“Hata nimeota nikiwa mbinguni.” “Sema kweli!”
“Kabisa!” Ulikuwa peke yako huko mbinguni?”
“Tulikuwa wengi sana” Tuseme mlikuwa katika hali gani?”
“Tulikuwa wote  tunafurahi na mimi niliweza kuwatambua wenzangu niliokuwa nikifahamiana nao duniani.”
“Mlikuwa na miguu na kila kitu?”  “Ndiyo lakini tulikuwa hatutembei; tulikuwa tunakwenda tu.”
“Ulimwona Mungu?”
“Hata! Isipokuwa tulikuwa tukifahamu kwamba kulikuwa na nguvu fulani juu yetu, ambaye nafikiri ndiye Mungu mpenzi.”
“Mlikuwa katika rangi gani?”  “Sikuona rangi.”
“Yaani hukutofautisha kati ya Mzungu na mtu mweusi.” “Mimi sikuona rangi.”
“Lakini Kalia kabla ya kwenda mbinguni lazima ufe.”  “Ndiyo.”
“ Unakumbuka jinsi ulivyokufa na  jinsi ulivyofanya safari yako ya kwenda mbinguni?”
“Ndiyo.” Niliwaona baba na mama wamezunguka kitanda changu, halafu baada ya muda nilijiona hali yangu imegeuka. Nilikuwa nikitangatanga mara nilipowaona wenzangu wanakuja kunipokea. Nilikuwa mbinguni tayari.
     “ Ulivyoona wewe mbingu hiyo mbali na dunia?”
    “ Hata! Mara fulani fulani Mungu mpenzi alikuwa anaturuhusu kuja ulimwenguni. Tuliwaona watu, lakini wao waliuwa hawawezi kutuona. Harafu tulirudi. Tulipokuwa tunafika mahali fulani mara hali yetu iligeuka tukajiona mbinguni tena. Hali hii ya kugeuka tulikuwa tumezoea kuiita ‘kupokelewa na Mungu mpenzi’.”
“Bado sijaelewa, yaani mliuwa mkitembea kwa miguu?”
“ Hapana, tulikuwa tunakwenda tu, halafu hali yetu  kuigeuka na tukajiona  mbinguni tena.”
“Mlikuwa mnakwenda tu namna gani?”  “Kwa nini wewe huelewi?”
“Kwa nini kila mara unasema Mungu mpenzi?”
“Kwa sababu tulipokuwa mbinguni tuliona kwamba Mungu anatupenda vile kwamba tuliona vigumu kumkosea kwa sababu ya aibu kubwa.”
Baada ya mazungumzo hayo; mtihani ulibaki kwa Kazimoto, kutafakari alioambiwa na Kalia kuhusu kufa na kwenda mbinguni. Alitafakari juu ya kufa, na alibaini kwamba kufa ni kugeuka hali “…yes, a change of state,”… nilisema kwa kiingereza, (Uk.75). Pia alibaini kuwa mbingu haikuwa mbali nasi. Vilevile waliokufa tuko karibu nao. Hatuwezi kuwaona kwa sababu hali yetu haijageuka. Jambo lingine ambalo alilitambua ni kuwa wale ambao hawatendi dhambi ndio wanaotambua kwamba Mungu anatupenda vile kwamba ni aibu kumkosea. Kuhusu watu ambao hutenda dhambi huishia motoni kama adhabu yao, ni suala ambalo alilikumbuka Kazimoto na kumuuliza Kalia: “…Asee, hukusikia kwamba kulikuwa na watu wengine motoni?”
“Hata! Sikusikia.”
Mwongozo tunaoupata kwenye sura hii, ni kuwa, maisha ya starehe duniani yanakuwepo, ila baadae yanaisha pale mtu anapokufa. Baada ya kufa maisha mengine yanasadikika kuwepo mbinguni, ambayo ni tofauti kabisa na maisha yale ya ulimwenguni. Ndipo tunaweza kujiuliza kwamba, maisha ni nini au kitu gani?


SURA YA 6
Sura ya sita ni sura ambayo inazungumzia namna ambavyo mtu huweza kuiga tabia mbaya kutoka kwa nduguye au rafiki yake hadi kuona maisha mabaya. Ni sura ambayo msimulizi anaeleza jinsi ambavyo Kalia alianza kuiga mambo ambayo alikuwa anaona kaka yake akifanya. Tunaelezwa jinsi alivyofikia hatua ya kumvamia na kumbaka msichana aliyekuwa anachunga ng’ombe, (uk.80-81).Lakini hayo yote Kalia aliyaiga kwa Kazimoto. Vilevile anasimulia ambavyo Kazimoto alimdharau Kabenga kwa tabia yake ya kuingilia mke wakati ana mke wake wa halali. Pia katika sura hii tunaambiwa kuwa Rukia hali yake ilianza kuwa mbaya sana kutokana na ugonjwa uliomsibu. Ndipo walipoitwa Tuza na Tegemea ili kumsaidia Rukia kwani alikaribia kujifungua: mama yake Rukia anagoma kula mpaka bintiye atakapojifungua,(uk.76). Chuki dhidi ya Manase inamkumba Kazimoto baada ya dada yake kukaribia kuijfungua kwa sababu ilikuwa mimba ya Manase na alimtelekeza Rukia.
Udhanaishi juu ya maisha yanarejea tena kwenye mawazo ya Kazimoto. Ni pale ambapo aliona nyuki anaanguka katika maji na kujaribu kujitetea ili kuona maisha yake. Alichukua jukumu la kuokoa maisha ya nyuki huyo kama tunavyoona; “ …Juu ya jiwe niliona kibwawa kidogo cha maji. Ndani ya maji haya niliona nyuki ameanguka akiogelea. Nilijongea karibu. Mwanzoni nilifurahi kumwona huyu mdudu akipigania maisha. Lakini baada ya muda mfupi nyuki alikata tamaa. Nguvu zilimwishia alisambaza mbawa zake, miguu yake ilianza kupiga pole pole kama mtu aliyekata roho. Huruma iliniingia moyoni. Niliona kwamba nilikuwa na uwezo wa kuokoa maisha yake kwa tendo moja  dogo tu ambalo lilikuwa haliitaji hata tone moja la jasho. Nilijiona Mungu mdogo. Nilitazama tena pande zote, watoto, nyumba na miti, vyote vilikuwa chini yangu.
Nilichukua kijiti kidogo sana ambacho kwacho nilimtoa yule nyuki majini. Mbawa zake zilipokauka aliruka bila kusema asante. Aliruka bila hata kujua nani amemwokoa. Kwa huyu mdudu nilikuwa na nguvu ambazo haziwezi kufahamika. “Labda mfano huu unaweza kumsaidia mwanadamu katika kuelewa fumbo la Mungu,” nilisema moyoni. “Lakini labda haiwezekani. Tuseme kama yule nyuki akinifikiria mimi kuwa mwenye uwezo usioeleweka sio kusema kwamba mimi ni Mungu, kuna mwenye uwezo zaidi kuliko mimi. Labda hata mwanadamu anaweza kusema kwamba kuna mwenye uwezo kuliko yule tunayemfikiria kuwa ni Mungu. Lakini kama ni vile tutakwenda nyuma mpaka wapi? Labda tunaweza kusema kwamba ni wakati. Wakati wenyewe ni Mungu maana haukuumbwa.”
Katika kutafakari jinsi alivyookoa maisha ya nyuki na kuyalinganisha na mwanadamu anavyohangaika: mara akilinganisha na uwezo wa uwepo wa Mungu, Kazimoto alichoka. Aliamua kuchukua kitabu na kujisomea: kilizungumzia maarifa na tamaa zinavyompeleka mtu katika mabaya na mazuri katika maisha yake. (Uk.79-80).
Kuanzia ukurasa wa (82), masimulizi yanahusu habari za kifo cha Rukia. Kabenga na Kalia ndio waliomfuata na kumpasha habari za kifo cha dada yake Kazimoto;
       “…Sikuona kwa nini walinikimbilia mimi kama kwamba mtoto alikuwa wangu. Waliponifikia Kabenga ndiye aliyekuwa wa kwanza kuzungumza. “ Kazimoto, ndugu yako ha… ako kati… katika hali mbaya sana. Nilikaza mwendo ili niwahi; nifike kabla hajaaga dunia. Kabenga alipoona kwamba sasa sauti zinaweza kusikika alinigeukia. Alinitazama usoni. Nami nilielewa.
    
“ Kazimoto,” alisema, “ndugu yako amekufa!” Niliinama. Uchungu ulionipata ulikuwa mwingi.
“Kazimoto,” Kabenga aliendelea huku akiweka mkono juu ya bega langu, “twende nyumbani; watu nyumbani wanakungoja wakupe pole ya msiba.”
Kazimoto alienda nyumbani na kukuta msiba. Alienda moja kwa moja katika chumba alimokuwa amelazwa marehemu dada yake. Alimshuhudia kwa kumgusa kwa mkono akiwa amelazwa kwenye kitanda. “…wakati huo huo machozi yalijaa machoni. Niliyaacha yatelemke.”
Baada ya kifo cha Rukia, mama yake Kazimoto, naye alizimia. Baba yake ndiye aliyemjulisha Kazimoto, … nilipotoka nje baba aliwaacha watu waliokuwa wamemzunguka wakimpa pole akaja kuzungumza nami. “Kazimoto, mama yako amezimia. Amelazwa upande mwingine alikuwa akimwagiliwa maji kichwani. Niliingia ndani ya nyumba tena. Chumbani alimokuwa amelazwa niliwakuta Tuza na Tegemea. Walikuwa wamekaa karibu naye. Mmoja alikuwa akimpepea kwa sahani; mwingine alikuwa akimwagilia maji kichwani. Nilipomshika mkono niliona kwamba moyo ulikuwa bado ukipiga ingawa bado kwa hafifu.”
Baada ya Kazimoto kushuhudia mama yake akiwa amezimia, alipewa wosia aliomwachia marehemu dada yake.
  “Kazimoto,” Tuza alisema, “ndugu yako amekufa kwa sababu amekosa nguvu; alikuwa hajala vizuri kwa muda mrefu uliopita.”
“Hayo usemayo ni kweli,” nilimwambia. “ Amekufa akitaja jina lako.”
“ Alisema nini kuhusu jina langu?”
“Alikulilia; akikuomba umsamehe kwa yale yote yaliyotokea kwake. Amekuomba usisikitike sana. Hata yeye alikuwa haoni tena maana ya kuishi.”
“Ndiyo hayo aliyosema?”
“Nimesahau jambo moja. Amesema kwamba, maadam yeye akitoweka kama yalivyokwisha kutimia, anakutakia uhusiano mzuri na Manase. Yeye amemsamehe ni zamu yako sasa kumsamehe.(”uk.83)
Kutokana na hali ya huzuni iliyokuwa imeikumba familia ya mzee Mafuru, usiku Kazimoto alianza kufikiri juu ya kifo. “Nilifikiri jinsi kifo changu kitakavyonijia – kwa ugonjwa, kwa ajali au kwa kukatwakatwa na wezi? Labda kwa uzee au kwa sumu! Huenda nikajiua mwenyewe! Nilikumbuka ndoto ya Kalia. Niliwakumbuka wale ng’ombe, sisimizi, nyuki na mengine mengi niliyoyaona huko machungani. Niliona kwamba adhabu kubwa ya mwanadamu ni maisha yenyewe. Nilimkumbuka mlevi mmoja niliyemkuta akipiga mti mweleka mpaka akaumia mwenyewe. Maisha ndiyo yaliyokuwa yakimsumbua wala si pombe. Wakati huo usiku niliyaona maisha kuwa chanzo cha yote. Sikuona kwa nini mwanadamu alicheza ngoma na kupiga vishindo chini. Sikuona kwa nini alicheza twisti mpaka utumbo ukakaribia kukatika. Kwa nini mwanadamu alijidai kupiga mpira kwa kichwa kitunzacho bongo, sikuona. Mwanadamu mwenye akili hufurahi apitishapo moshi puani! Kweli, kama sigara za aina fulani zikitengenezwa , sigara ziwezazo kupitisha moshi masikioni, mwanadamu atanunua na kupenda hizo zaidi kuliko za siku hizi? Yote mwanadamu mwenye akili anafanya kwa jina ambalo limepumbaza akili. Jina ‘Furaha’ ambalo ni neno jingine la adhabu.
      Hii ni adhabu ambayo kila mwanadamu amepewa – kutunza maisha yake. Maisha ambayo hayashibwi wala kuridhishwa. Zaidi ya hayo mwenye nguvu anatunyang’anya maisha haya wakati wowote bila hata kutuarifu. Kweli, mfano wa adhabu hii kali ni yule mtu aliyeamrishwa kujaza maji ndani ya pakacha. Na sisi wanadamu tumekubali kufanya hivi kwa jina la ‘Furaha’. Maisha matamu! Yaani adhabu ni tamu. Ndiyo kusema tuna akili kweli wanadamu? Maswali haya yalinizunguka sana kichwani. Mara fulani niliamua kwamba mwanadamu hana akili. Kama angekuwa na akili angekataa adhabu hii; na kama yule ambaye ametupa adhabu hii angetushurutisha tungejua sote. Mara zingine niliona amfuata. Mwanadamu amekusudia kuacha adhabu hii.  Mwisho wa mwanadamu utaletwa na mwanadamu mwenyewe. Vita vya kwanza vilishindwa kuleta mwisho huu. Vita vya pili pia vilishindwa. Tegemeo sasa ni vita vya tatu au vya nne. Wakati usingizi uliponichukua, sikumbuki.”( Uk.84-85).
Kauli ya ‘maisha hayana maana’ ilizidi kujidhihirisha kwa Kazimoto: ni wakati mama yake alipokufa siku iliyofuata baada ya kifo cha Rukia. Ilikuwa ni siku ya kuzika mwili wa Rukia ambapo mama yake Kazimoto alilia kwa ukali na huzuni kwa mwanae. Uk.85: Wakati wa kuchimba kaburi, mama alikuwa ndani ya nyumba akiongea mambo ambayo yalikuwa hayaeleweki. Lakini kaburi lilipokwisha, Tuza na Tegemea walimshika na kumsaidia kutoka nje ili aone binti yake akizikwa. Alipofika tu mlangoni na kouna shimo lililokuwa limechimbwa tayari kumzika binti yake alilia kwa sauti ya juu sana . “Rukia! Rukia!” hali akionyesha kwa mkono wake kaburi. Halafu alia- nza kulia kwa namna ya pekee. “Kichwa! Kichwa!’ alitotoma na kuanguka chini. Wakati alipobebwa kupelekwa kitandani alikuwa amekwisha kufa. Kifo chake kilipotangazwa kila mmoja alishangaa. Huo ndio ulikuwa mwisho wa mama yangu. Nilikuwa siwezi kumuona tena maishani. Nilikuwa siwezi kusikia tena sauti yake. Mola alimnyima ile furaha kubwa wapatayo akina mama wakati mtoto anapooa. Huo ndio uliokuwa mwisho wa mama aliyempenda binti yake wa pekee kama pumzi na mwanadamu. Alikuwa amenyang’anywa pumzi yake. Niliyakumbuka tena maneno yake: “Kazimoto,tuache tupumzike tuache tulie. Huu ni ugonjwa umeletwa na vijana, na utatumaliza sisi kina mama wenye mabinti. Ninajiona kwamba nitakwenda na binti yangu.”
Katika mwendelezo wa sura hii, mwandishi anamlizia kwa kutuonesha kuwa ndugu wafiwa walipekekwa na watu wailokuwa wamekuja kuwaanali kwa msiba, ili kuwaliwaza. Walipelekwa katika sehemu za kunywea pombe. Walinunuliwa pombe na watu hao. Ndipo tunapoona mawazo ya kulipiza kisasi yanaibuka tena kwenye mawazo ya Kazimoto. Safari hii ilikuwa ni malipizo kwa Kabenga. Kwa sababu vifo vya ndugu zake Kazimoto, vilitokana na Manase mtoto wa Kabenga ndio maana Kazimoto alitaka kulipiza kisasi. Alifanya hivyo, baada ya jaribio lake la kumuua Kabenga kushindikana sababu ya woga wake: ndipo alipoamua kuchoma nyumba ya mzee Kabenga. (Uk. 87-89).

SURA YA 7.

Ni mwendelezo na msimamo au mtazamo ule ule uliotumika kuandika riwaya hii katika visa vyake. Ni juu ya jambo moja la maisha ambalo lilikuwa likumsumbua kijana Kazimoto pia katika sura hii ya Saba. Kudhihirisha hilo soma maneno yafuatayo kwenye uk.90:
      “Nilipofika mtoni sikukuta mtu. Nilikaa kwa muda nikiyatazama maji yakitelemka kuelekea ziwani. Niliaza kufikiria kama kweli maisha ya binadamu hayawezi kulinganishwa na maji yatelemkayo kutoka mlimani kuelekea ziwani au baharini. Maji yalikuwa yakitelemka kwa kasi sana; kurudi juu yalikuwa hayawezi. Yalikuwa hayasukumwi na nguvu kutoka nje isipokuwa yalikuwa yakinda tu kwa sababu kulikuwa na mteremko. Yatake yasitake yalipaswa kuteremka. Nilishangaa kuona kwamba watu wengine wamelinganisha maisha ya binadamu na mtu apandaye mlima akisukuma jiwe na kurudi nyuma kuokota jiwe. Niliona kwamba mwanadamu anateremka kama maji kwa kasi sana; na kama maji ya mto yakusanyavyo takataka za kila aina ndivyo mwanadamu akusanyavyo taka wakati wa maisha yake. Maji yakifika ziwani yamekwisha kusanya taka nyingi; pia mwandamu afikapo mwishoni mwa maisha yake huwa amekusanya taka kadri ya muda alioishi. Niliona heri ningekufa ningali mtoto.”
Kazimoto anaendelea na tafakari yake juu ya maisha, kwa kutoa mifano ambayo sio rahisi mtu kuielewa haraka bila kuitafakari kwa kina. “Nilipokuwa nikivua nguo zangu niliona mjusi akiwa amejibanza kati ya ufa wa jiwe. Yeye alifikiri nilikuwa simuoni.  Nilikwenda pole pole na mara nilikata mkia wake. Mjusi alijisukuma ndani. Mkia wake ulianguka chini. Ulipapatika. Nilishangaa, kwani maisha yote alikuwa nayo mjusi aliyekuwa ndani. Sikuona kwa nini mkia uliruka kwa muda mrefu vile kama kwamba ulikuwa bado umeungana na mjuisi. Nilijitumbukiza majini. Baada ya kuoga niliona mkia ukiburuzwa na mamia ya sisimizi kuelekea kwenye kishimo kidogo.”uk.91.
Masimulizi sasa yanaingia katika mtazamo mwingine ila unaolenga ujumbe ule ule na msimamo ule wa msimulizi. Kazimoto anasimulia maswahibu yaliyomkuta mdogo wake Kalia: alipouwa sasa amejiingiza katika tabia mbaya sana bado ni mdogo. Kalia alichukua hela ambayo ilisahaulika ndani ya nyumba pale baba yake alipokuwa akihesabu pesa zake. Alikuwa akimchukulia Tegemea pesa baada ya kuwa naye kimapenzi hali Tegemea alikuwa mama mkubwa wa kumzaa. Kitendo hicho cha kuchukua hela kilimponza Kalia baada ya kuonwa na baba yake na kupigwa vikali na baba yake (uk.91-92). Katika ukurasa wa (93) kituko kingine kinasimuliwa: kilimhusu Kazimoto. Ni baada ya mama yake Vumilia, Tegemea; kuwavamia mzee Mafuru na familia yake kwa malumbano ambayo yalikuwa ni kuhusu Kazimoto kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Vumilia mtoto wake Tegemea hali akijua kuwa alikuwa akiozeshwa kwa Manase. Kazimoto alionywa vikali na babayake, baada ya kukiri mwenyewe kuwa alikuwa akitembea na Vumilia. Uk.94-95.
Masimulizi yalihamia kwa Kalia. Muda huu Kalia alibainika akijirusha na Tegemea. “Kweli Kalia alikuwa akifuata nyayo zangu; niliona aibu kwa jambo nililolitenda. Kalia alikuwa haendi kwingine isipokuwa nyumbni kwa Tegemea. Badala ya kupitia mlango wa nyuma yeye alipiti mlango wa mbele. Kweli, Kalia alikuwa sasa akinipitia katika mambo yangu. Mimi nilizoea kupitia mlango wa nyuma. Alipoingia nilitembea pole pole kuelekea nyumba ya Tegemea. Nilijibanza ukutani. Mimi nilifikiri kwamba alikuwa akimtongoza Vumilia. Nilishangaa kumsikia akiongea chumbani mwa Tegemea.
         “ Umemaliza kuvua?” Tegemea aliuliza. “ Tayari,” Kalia alijibu.
         “Njoo tulale.”
      “Huna haja ya kunikaribisha.” Nilisikia Kalia akirukia kitandani. Kijana mbichi!
     “Angalia usivunje kitanda changu.”
     “ Shuka zaidi upande huu; mgongo wangu uko nje.”
“Unafahamu kwa nini Kalia nakupenda?”  “Niambie!”.
“ Unanikumbusha siku zangu za zamani nilipokuwa nikitembea na vijana wadogo kama wewe. Mimi huwa nafurahi kuona kijana mzuri akiruka ruka juu ya kifua changu. Huwa kama ninanyonyesha mtoto mdogo. . . haraka gani Kalia; mimi nipo kwa ajili yako.”uk.96-97.
Umdhaniaye ndiye, kumbe siye; kikulacho kinguni mwako. Misemo hii ilijidhihirisha kwenye sura hii, pale ambapo mchawi aliyekuwa akiisumbua familia ya mzee Mafuru alipojulikana. Alikuwa ni jirani yao, mzee Kabenga. Kalia alimjulisha Kazimoto.
“Nilipofungua nilimwona Kalia. Kwa muda mrefu tulikuwa hatujazungumza  vizuri, hasa siku ile niliyomwambia kuwa alifanya vibaya kuiba shilingi zangu.
“ Nina mambo ya kukwabia.”alisema.
“ Ingia ndani.” Aliingia. Niliwasha taa. Alikaa juu ya kiti, name nilikaa kitandani, shuka yangu imenizunguka.
“ Kazimoto, nimevumbua siri kubwa.’ Siri gani?’
“ Nimemfahamu yule aliyekuwa akitupia mchanga wakati wa usiku.” ‘Nani?’ “..Kabenga.”
“Wewe umefahamuje?” Alicheka kidogo.
“Kazimoto, siku hizi katika mambo ya wanawake nakuzidi wewe. Kwa muda nilikuwa nikimwendesha Tegemea . . . Tegemea siku moja aliniambia siri yake na Kabenga. Siri yenyewe ni hii: Kabenga ni marafiki wa muda mrefu. Tegemea siku moja alimwomba Kabenga shamba la kulima pamba. Kabenga alimwambia kwamba alikuwa na mashamba mengi sana. Lakini kwa bahati mbaya serikali ilimleta baba kuishi humo kwa kuwa alkuwa hayatumii yote. Kwa hiyo njia ilitafutwa ya kutufanya sisi tuhame ili apate kumpa Tegemea mashamba haya. Nami naona habari hii ni ya kweli.” Uk.98-99.


SURA YA 8.

Ndani ya sura ya nane, tunapata kusimuliwa maisha mengine yahusuyo kijana Kazimoto. Lakini hapa maisha hayakuwa ya Kazimoto peke yake, vilevile yalimhusu pia msichana Sabina. Sabina alikuwa msichana mbichi jirani na akina Kazimoto, ndugu yake Manase na mtoto wa mzee Kabenga na Tuza. Kazimoto anaeleza jinsi ambavyo Sabina alivyokuja kutoka Tabora alipokuwa anafanya kazi ya kufundisha: na alikuja kumpa pole Kazimoto kutokana na msiba ulitokea kwao. Ni miongoni mwa wanafamila ya mzee Kabenga ambao walikumbwa na kisasi cha Manase. Sura hii pia inadadavua zaidi mawazo ya Kazimoto baada ya kukutana na Sabina. Kama ilivyokwisha simuliwa, Kazimoto sasa alitaka alipize pia kwa Sabina kama alivyofanya Manase kwa Rukia dada yake Kazimoto.
Kazimoto alindelea na mawazo yake ya kutaka kulipiza kisasi kwa Sabina. Uk. 102: anasema, “ Ng’ombe mzee akikanyaga matopeni harudi mpaka achinjwe pale pale. Hapa sasa kulikuwa na ng’ombe mzee. Kazi yangu ilikuwa ni kumsukuma matopeni, na kumwacha akitapatapa roho ili kumaliza siku zake za mwisho. Manase alimtia mimba ndugu yangu, akafa. Ngugu yake sasa alikuwa karibu nami. “Kwa nini nami nisifanye kama yeye?” nilijiuliza. Yeye mwenyewe Manase mtoto wa Kabenga, alisema mimi mwanaume kama yeye. Nami, mtoto wa Mafuru, nilikata shauri kutumia njia yoyote ili kumpata huyu msichana, sio kumpata tu kwa siku moja, isipokuwa mpaka nihakikishe kwamba tumbo lake lilikuwa zito.”
Sabina ni msichana ambaye alikuwa ameanza tayari kukata tamaa ya kuolewa. Alikuwa ni msicha ambaye umri wake ulikuwa unaelekea kukosa mchumba. Alikuwa na miaka 26. Sababu ya kufikisha miaka yote hiyo bila mchumba ni kwamba, alikuwa ni msichana aliyefuata sana dini na wavulana waliomfuata aliwajibu kwa majibu yenye kurejelea bibilia. Pia walimwona kuwa ni mwenye kiburi na aliyewadharau wanaume. Wanaume wengi walimkimbia baada ya kuona hawapati cho chote isipokuwa maneno. Sabina alikuwa ameanza kukata tamaa ya kuolewa na aliamini kuwa Mungu alikuwa akimjaribu yeye na alikuwa hataki kupoteza imani yake, (uk.100 na uk.103-104), Kazimoto anamuuliza Sabina kinachomfanya asiwe na mume. Na Sabina anamjibu. Katika majibizano hayo tunaona Sabina mbali na kumwamini Mungu, tunaona anasema kuwa ana machungu ya kutoolewa na ana huzuni moyoni.
Zaidi masimulizi yanazidi kutuonesha Kazimoto anavyojitahidi kumpata Sabina msichana aliyekuwa mzuri mnene na mfupi kiasi. (Uk.106,107,108,109). Sabina tayari ameshakuwa wa Kazimoto na ni wapenzi wasio weza kuitilafiana. Mapenzi yao sasa yalinoga hadi Sabina akawa anamfulia na kunyooshea nguo Kazimoto. Jambo ambalo lilimfanya Kazimoto kumsahau kabisa Vumilia: wazo la kulipiza kisasi liliitika kichwani mwake, uk.109, Kazimoto anaonyesha mapenzi ya dhati kwa Sabina, anakimbia kwenda kumuona baada ya Kabenga kuwataarifu kuwa hali ya Sabina imekuwa mbaya, na aliumwa ghafla. Mapenzi sasa yalinoga sana na Kazimoto anaamua kumchumbia Sabina ili awe mkewe, uk.113.
Wahenga walisema, “Asiyefunzwa na mama yake, basi ulimwengu humfunza.” Ni methali yenye maana yake ambayo ukweli huu ulijidhihirisha kwa Kalia. Kalia aligeuka na kuwa Nunda mla watu pale kijijini. Kalia alianza tabia ya kuwavamia wanawake usiku na kuwalazimisha kufanya nao mapenzi: waliokataa aliwatishia kwa visu na silaha ili wakubaliane naye. Baada ya kugundulika, Kalia alifukuzwa kijijini. Kuanzia hapo kila mtu akawa anamwinda yeye, kwani amekuwa tayari ni adui wa kila mtu, (uk.110 – 111). Nadharia ya maisha hayana maana yoyote ilionekana kuwa na mantiki kubwa sana: ni baada ya kusikia habari za kifo cha Kalia. Japo alkuwa adui wa watu kwa muda ule Kalia mwili wake ulikutwa unaelea majini huko mtoni.
“Mna habari?” Kabenga alianza kusema. “Mwili wa Kalia umekutwa ukielea majini huko mtoni kwa siku mbili.” Watu wameuona, lakini hakuna mtu apendaye kujiweka hatarini. Mwishowe nimejitolea kuja kuwaambia. Heri twende tukautoe kabla haujaharibu maji yote ya mtoni, watu wakakosa mahali pa kuoga.” Uk.114. ndivyo kifo cha Kalia kilivyojulikana pasi na mtu kujua amekufaje. Na katika mazishi ya mwili wa Kalia watu wachache walihudhuria mazishi hayo; hasa familia ya mzee Mafuru na mji wa Kabenga ndio walioshiriki kikamilifu kwenye maziko hayo kwa sababu alikuwa ndugu yao.

SURA YA 9
Kazimoto bado anaendelea kutazama kwa jicho pana na anajiuliza juu ya maisha ya mwanadamu na hapati jawabu lake kwa urahisi. Anazidi kutuonyesha misukosuko inayomfanya mwanadamu kuyajutia maisha. Uk.115, anaeleza jinsi ambavyo Tegemea alivyokutwa anaiba viazi kwenye shamba la Mafuru. Mafuru anamsamehe Tegemea kwa kuona kwamba aliiba kwa sababu ya njaa ya chakula. “Swali hili, baba alilikatisha upesi kwa kuwaambia wasijali sana. Halikuwa jambo baya kumsaidia mtu mwenye njaa walau siku moja.”
Vilevile anajaribu kujiuliza juu ya mwanadamu na akili zake. Anasema kuwa mwanadamu akili zake ni fupi, uk.116. Mfano unatolewa kuudhibitisha kuwa binadamu akili yake ni fupi, akimwelezea kijana ambayea alipita katika njia ambayo ilikuwa imezibwa kwa miiba ili watu wasipite. Kijana huyo alilazimisha kupita na kukutana na joka kubwa ambalo lilimdonoa na akafa pale pale. Ndivyo anavyomfananisha mtu anayejiuliza maswali juu ya Mungu na kujaribu kumchunguza Mungu. Maisha hubadilika. Ndivyo anavyobadilika Kazimoto; baada ya kuona kwamba barua aliyomwandikia Manase kwa hasira ya kulipiza kisasi haikuwa na maana tena, bali ni kumuomba samahani Manase na Manase anamsamehe,( uk.117).
Kazimoto akiwa tayari ameshafika kwa Manase na sasa ni mgeni wao: anashuhudia mzee aliyekuwa ni mfanyakazi wa ndani akikaripiwa na Salima mke wa Manase. Ni mzee ambaye ki-umri ukilinganisha na Salima hakupaswa kukaripiwa na kijana mdogo kama Salima ijapo ni mfanyakazi wake. Uk.120. Bado suala la maisha linazidi kuumiza kichwa cha Kazimoto; tunaona linajitokeza tena katika mazungumzo yake na wenyeji wake. Wanaongelea juu ya wanawake wanaojiremba na kujiangalia kwenye kioo kila mara, pia na watu ambao ni wasomi lakini hawachani nywele. Katika kutafakari maisha, Manase analeta mada ambazo mifano yake inagusa maisha ya binadamu, pia zaidi katika imani ya Mungu. Wanajadiliana namna Yesu alivyokufa, Kazimoto anasema Yesu alijiua kwani alijua kwamba atakufa. Hivyo alijiua akiona, Salima anamjibu kuwa anahitaji imani, uk.122. Wazo la kifo na mwisho wa mwanadamu, linazidi pia kujitokeza tena katika mazungumzo. Kazimoto ansema kuwa kufa ni kugeuka hali. Na kama kufa ni kugeuka hali basi mtu baada ya kufa anageuka tena kwa mara ya pili. Swali linaloleta dhana ya maisha baada ya kifo kuwepo. Uk. 123. Katika uk.124, ndipo uwepo na kutokuwepo kwa Mungu unazungumziwa hapa kama ambavyo tumekwisha ona katika utangulizi wa uchambuzi wa riwaya hii.
Vilevile suala la mbingu linajitokeza katika mazungumzo. Ndipo tunapomwona Manase akimuuliza Kazimoto kuhusu mbingu. “Tuseme wewe unafikiri nini juu ya mbingu?” Manase aliniuliza. Swali lenyewe sikulielewa vizuri. Hata hivyo nilijaribu kumjibu. Mwanadamu ni kiumbe ambaye amejaribu kutafuta mbinu nyingi ambazo zilimwezesha kupata furaha. Kwa kuwa ameshindwa kupata furaha hapa duniani amejenga kichwani kitu kama mbingu, yaani mahali ambapo anategemea kupata furaha baada ya kufa.”
“Kwa hiyo wewe umeona kwamba wazo la mbingu limeletwa na kushindwa kwa mwanadamu kupata furaha hapa duniani.”
“Ndiyo.” Tulinyamaza kwa muda.
“ Na kwamba ni hali ya kujitakia jambo jema tu.”
“Kabisa.”
“Je wewe unaona kwamba mbingu ipo au haipo?”
“Ninaona vigumu uamini kwamba ipo……” Udhanaishi. Uk.122 – 124, mambo na mtazamo wa kuwepo kwa mbingu na Mungu unasumbua vichwa vya watu watatu: Kazimoto, Manase na Salima. Pia uk.125.
Mambo ya kijamii yahusuyo maisha ya binadamu yanajadiliwa. Ni mambo ya kifamilia na mahusiano zaidi. Suala la uaminifu katika ndoa linajadiliwa kwa mitazamo mbalimbali ya wahusika hawa watatu. Inafikia muda fulani wa kutoelewana kidogo kati ya Manase na Mkewe Salima, uk.126 – 127. Mwanadamu sasa anagusiwa juu ya uzuri na ubaya wake. Na ni mada anayoileta Kazimoto, izungumzwe mezani. Kazimoto anauliza: “Wewe unafikiri nini juu ya ubaya na uzuri wa binadamu?”
“Mimi ninaona watu wabaya ni wale niwachukiao,” Manase alidakia mara moja. Ninachukia  wale watu wanaojidai kwamba wao ni wajuzi wa kila kitu. Hawa ndio waletao chuki duniani. Kama ulivyosema mwanadamu si rahisi kueleweka…”uk. 127 – 128. Pia hapo hapo mada inayohusu vijana wadogo kuijiingiza kwenye mapenzi wakiwa na umri mdogo inaingizwa na Kazimoto, na inajadiliwa kwa kila mtu kutoa mtazamo wake. Kazimoto anauliza, “ Unafikiri nini kisa cha ugonjwa huu, Manase?” nilimwuliza .
“Ugonjwa gani?”aliniuliza.
  “Huu ugonjwa wa vijana kuanza mchezo mbaya wangali umri wa miaka kumi na miwili na mara zingine kujazana mimba ovyo na kuharibiana maisha. Unafikiri kitu ganai kimeleta mambo haya  kwa haraka namna hii au labda unafikiri ulimwengu umegeuka, basi?”
“Mimi ninaona kwamba sababu kubwa ni kwamba ndoa imepoteza maana yake. Zamani jambo la maana ambalo kila mwanadamu alikuwa akitegemea maishani  lilikuwa ndoa. Lakini siku hizi kama elimu na pesa yamezuka na ndoa imekuwa kama kitu kisicho na thamani. Vijana wako tayari kuahairisha ndoa, lakini wasome, ingawa wana umri wa miaka thelathini au zaidi. Unafikiri wakati wote huu watakuwa wanafanya nini? Hawawezi kukaa kama mabikira.”
 “ Wewe huoni kwamba ndoa imepoteza maana kwa sababu ya vijana kuchezeana wangali bado watoto wadogo, kabla hata ya kufahamu mambo mengi ya maana usemayo?” Manase hakujibu swali langu vizuri, lakini wakati huu Salima aliingilia kutoa mawazo yake.
  “Mimi ninaona kwamba sababu kubwa ni malezi ya nyumbani. Malezi ya nyumbani yamelegea kupita kiasi. Licha ya malezi mabaya kuna hii hali ya wasichana wadogo kutembea na dada zao. Msichana atafanya mambo yale yale aliyoyaona dada yake akifanya wakati wakitembea pamoja. Mvulana pia atafanya hivyo hivyo. Itakuwa vigumu kuondoa uovu huu sasa kwa sababu kizazi kimoja kinafunza kizazi kinachofuata.”
 “ Ndiyo Manase alisema kwamba uovu umo ndani yetu sisi,” alidakia….”( Uk.128 -130).
Katika sura hii hitimisho linaongelea maisha ya mwanadamu yalivyo hatarini muda wote, na kusema kwamba binadamu anatembea na kaburi lake kichwani kama anavyofanya konokono: ingawa mwanadamu anajiweka kichwa kichwa na kujiona anaweza na yuko sawa bila tabu yo yote. Binadamu anashindwa kulifahamu hili wakati konokono anakuwa mwelewa juu ya hili jambo. Mwisho kabisa wa sura hii tunaona barua ya Kazimoto aliyoandikiwa na Sabina wakitegemea kuoana na tayari ni wachumba. Uk. 131.


SURA YA 10
Sura ya pili imeisha kwa kuona barua ya Sabina kwa Kazimoto: iliyokuwa ikimtaka Kazimoto kupendekeza mwaka ambao wapendanao hao, wataoana. Hadithi hii inaendelea kuzungumzwa na Kazimoto katika sura ya kumi. Kazimto anasimulia jinsi ambavyo yeye alikuwa akichukia uchumba wa muda mrefu ila alibadili mawazo hayo, baada ya kupokea na kuuelewa ushauri wa mchumba wake, yaani Sabina. Kazimoto aliona ni vyema kusubiri kama alivyoshauriwa na Sabina, uk.132.
Mara kwa mara katika kipindi hicho, Kazimoto alikuwa anakwenda mara kwa mara kijijini kwao. Mabadiliko fulani yalikuwa yamekwisha anza kutokea. Miongoni mwa mabadiliko hayo yalikuwa ni kuolewa kwa Tegemea na Kabenga. Tegemea aliolewa na Kabenga, na tayari alikuwa mke wa kabenga: kijijini wote walimfahamu kama mke wa Kabenga. Waliishi maisha ya ndoa kwa kufanya shughuli za kiuchumi; kama kulima, ambapo tunaona Tegemea hakuzoea maisha hayo ya shida kidogo. Alikuwa hajui kulima na aliona taabu kufanya hivyo ila alilazimishwa kulima na Kabenga kwa sababu ya uzembe wake. Tunaona malumbano yanatokea kati yao wakiwa shambani, hadi kupigana:
   Umeolewa ama hukuolewa? Wewe sasa ni mke wangu nafanya nitakavyo! Unakaa chini!” alikemea Kabenga.
  “ Mimi siwezi kulima! Kama ni chakula mtaninyima!” Tegemea alijibu.
 “ Utalima!”
 “ Mimi nimesema siwezi!”
  “Nimesema utalima na utalima!”
 “ Kama mambo ni hivi mimi nakwenda nyumbani!”( uk.134)
Hayo ndiyo maisha aliyoanza nayo Tegemea kwenye ndoa yake. Baada ya kuanza na furaha anakutana na msemo usemao ‘mwanzo huwa ni mgumu’. Hizo ndizo karaha za maisha – maisha ni mateso na maangaiko pamoja na vurugu, baada ya kuwa raha na furaha (utamaushi).
Pia badiliko jingine lilikuwa ni kwenye familia ya Mafuru ambapo tunaambiwa kuwa Mzee Mafuru alioa mke mwingine baada ya kufiwa na mke wake. Mama huyu wa kambo kwa Kazimoto, aliitwa Nzura, uk.136. Vilevile badiliko jingine lilikuwa ni Manase kuamishwa kituo cha kazi. Lakini Kazimoto anazungumzia mke wake Manase alivyojifungua mtoto na mtoto huyo alikuwa wa ajabu kidogo. Pia badiliko jingine lilikuwa ni kwa Kamata aliyekuwa amehaguliwa kuwa mwanangwa wa kijiji cha Saku. Baada ya miezi mitatu Kamata alijenga nyumba nzuri yenye bati, uk.137.
Katika uk.138, msanii anatuonyesha tukio ambalo lilitokea. Tukio hilo lilikuwa linaongelea namna ambavyo Kazimoto alikuwa akijiandaa kuanza kutangazwa kwa ndoa yake kanisani. Malumbano yalitokea kati ya Kazimoto na Padri, pale ambapo padri alikuwa akizozana na Kazimoto juu ya kutangaza ndoa yake kanisani ilionekana kuwa padri aligoma kidogo kufanya hivyo kwani kuna hatua ambazo zilikuwa zimekiukwa kabla ya kuanza kutangaza ndoa ya hao wapendanao. Pia tunaona ambavyo Kabenga alidai mahari makubwa kuzidi uwezo wa familia ya mzee Mafuru. Jambo ambalo lilileta kutoelewana baina ya Kabenga na Mafuru. Masimulizi yanaendelea kuongelea juu ya mazungumzo ya Kazimoto na Sabina kuhusu watakavyofanya ndoa yao, uk. 139-143.
Palipo na mafanikio, hakika vikwazo haviepukiki. Ndivyo ilivyokuwa kwa uchumba wa Kabenga na Sabina. Mtu mabaye hakujitambulisha alikuja na taarifa mbaya juu ya Sabina lakini lengo lake likiwa ni kutaka kuvunja uchumba wao . . . nilipokaa na baada ya kumsalimu yule mgeni, baba alisema, “Kazimoto, kuna jambo moja tu ambalo ninataka kufahamu. Na ninataka uniambie ukweli kabisa. Uongo haufiki mbali nami. Ninataka uniambie ukweli kabisa. Je, umekwisha kata shauri kabisa kumwoa Sabina?”
“Nisingekuwa nimekata shauri nisingekuwa nimekusumbua namna hii. Kazi yote umekwisha fanya; ninawezaje kubadili nia sasa?”
“Sitaki maelezo, wala sitaki uniulize mimi. Niambie kama umekwisha kata shauri kabisa ama bado.”  “Nimekwisha kata shauri.” Nilimjibu.
“Sijui utasemaje sasa. Kuna mgeni hapa amekuja na siri kubwa.” Nilimtazama mgeni.
“Wewe ndiye Kazimoto?” aliuliza. “Ndiye,” nilimjibu
“Wewe ndiye unataka kumuoa Sabina?” “Ndiyo.”
“Uchumba wenu ulianza lini?” “Miaka mitatu imepita sasa.”
“Unafahamu habari zozote kuhusu maisha yake huko Tabora?”
Kidogo tu. Lakini habari kamili sina.” ‘Hufahamu?’  “Sifahamu sana.”
Mimi Sabina ni jamaa yangu hasa na baba’ke amekwisha fika nyumbani kwangu kuleta posa.” ‘Jina lako nani? nilimwuliza. Alinyamaza kwa muda mfupi halafu aliniambia, “Fungameza”.
“Sabina ni nani kwako?” nilimwuliza tena.
Ujamaa wenyewe ni wa mbali kidogo, na sidhani kwamba unaweza kuelewa kwa urahisi hata kama nikikueleza. Ni jambo la maana sana. Hili jambo ndilo limenifanya nije hapa wakati kama huu . . . Fungameza anaendelea kueleza mambo mabaya na tabia mbaya ambazo anasema kuwa Sabina alikuwa akizifanya kipindi yuko Tabora. Miongoni mwa tabia hizo ni kwamba alishawahi kuolewa na jambazi ambaye alikuwa akimfungia ndani. Pia anaeleza habari za ukoo wake, akisema kuwa babu yake Sabina alikufa kwa ukoma na nyanya yake alikuwa mchawi. Vilevile anasema kuwa Sabina alitoa mimba mara mbili akiwa huko Tabora . . . UK. 145-147.
Pamoja na vizingiti alivyojaribu kuviweka bwana Fungameza, ila ndoa ilifanikiwa kufungwa kati ya Kazimoto na Sabina: wapenzi waliopendana. Masimulizi yanaelezea vizuri jinsi watu hao walivyofunga ndoa yao kuanzia ukurasa wa 149 hadi 151. Pia tunaambiwa kuwa baada ya shughuli za sherehe kumalizika katika miji ya Mafuru na Kabenga, siku tatu bibi harusi na bwana harusi, sasa walihamia kwenye makazi yao wenyewe walipokuwa wanafanya kazi zao. Kuondoka kwao huko kuliambatana na nasaha za mzee Kabenga kama mzazi wa wanandoa hao; hasa zaidi akiwaasa juu ya maisha yao ya ndoa, uk. 151 – 152. Kazimoto anaeleza jinsi walivyofika kazini kwao kama maharusi wapya na kupokelewa vizuri kwa shangwe na walimu wenzao.  Kama ilivyo kawaida kwa Kazimoto, udhanaishi ulimjia tena kichwani mwake na kuanza kujiuliza juu ndoa yao. Kazimoto anasema: “Kweli sasa nimeoa! Sasa nimepata faida gani?” Mbona mimi ni Kazimoto kama zamani. Sioni tofauti kati yangu na watu wengine, isipokuwa kuambiwa ‘mkeo hajambo?’ kila asubuhi na popote niendako. Mke wangu aniita ‘bwana’ngu’, kama kwamba yeye amenichukua. Nani sasa amechukua mwingine? Tumechukuana. Ndiyo, tumechukuana lakini mimi bwana yeye bibi. Kuna tofauti gani kati ya bwana na bibi?”. . . Uk,153.
Kila lenye mwanzo huwa halikosi mwisho. Ndivyo inavyodhihirika katika uk, 154, pale ambapo uadui uliokuwepo baina ya Kazimoto na Manase, pia kati ya familia ya Mafuru na Kabenga mgogoro huu ulikuwa juu ya mashamba. Barua kutoka kwa Manase inamfikia Kabenga ambayo lengo lake lilikuwa ni kushirikiana pamoja ili kuweza kuboresha kipato cha familia zao na kuondoa uadui huo. Ifuatayo ni barua ya Manase kwa Kazimoto;
    “ Bwana Kazimoto,
     Sikuweza kufika harusini kwa sababu ya matatizo fulani ya mke wangu Salima ambaye, anaendelea kukonda kila siku. Sababu inayomfanya akonde hivyo siijui. Tumejaribu dawa za hospitali lakini hazifai. Hakika ukimwona sasa utamsahau. Mimi sijui nifanye nini ili nipate kumrudisha katika hali yake ya zamani.
       Nafikiri litakuwa jambo zuri kama mtaweza kututembelea likizo ya Desemba. Labda nyinyi mtaweza kumtuliza. Jambo la pili ni hili: nasikia  baba’ko  na baba’ngu siku hizi wana uhusiano mzuri sana. Mji mmoja ukikosa mboga kwa siku moja  unakwenda kuchukua kwa jirani. Jirani akichinja ngo’mbe anapeleka mguu mzima kwa mwenziwe. Zaidi ya hayo wanasaidiana sana wakiwa taabuni.  Na ninasikia kwamba watoto wa kwenu wamezoea kwetu vile kwamba mgeni akifika ni vigumu kutambua  ni watoto  wa mji gani. Kwa hiyo ili kufanya mgogoro wa mashamba usahaulike kabisa tunaweza kujaribu kuwafanya walime pamoja .  Mimi ninapeleka shilingi mia tatu, wewe pia ukiongeza kiasi hicho, tunaweza kuwasaidia kulimisha shamba moja kubwa kwa trekta. Sina mengi.”
Haya ni mawazo mazuri ya Manase yaliyokubaliwa na Kazimoto pamoja na mkewe Sabina ili kuweza kumaliza kabisa mgogoro wa familia zao wa zamani. Matatizo mengine yaliikumba nyumba ya Kazimoto, baada ya kazimoto kutoka shuleni akakuta mkewe analia. Sababu ilikuwa ni kwamba alipokea barua ya mpenzi wa zamani wa Kazimoto ambaye anaitwa Pili, uk,156. Pia Kazimoto alipokea barua fupi iliyotoka kwa Vumilia:
   “Nasikia kwamba umemwoa Sabina. Hayo yote kwangu ni sawa. Lakini siwezi kuficha kwamba nikiwa naishi hapa duniani nitakuchukia daima. Sina mengi, isipokuwa kuwatakieni heri na fanaka katika maisha yenu.”
Kazimoto anasema hivi juu ya barua hii: “Barua hiyo niliisoma mara mbili. Niliona kwamba labda chuki haitakwisha kamwe ulimwenguni. Chuki itakanyagwa na mapenzi, lakini itajitokeza tena katika umbo jingine”, uk, 158.


SURA Ya 11

Kama ilivyo kawaida ya jamii nyingi duniani na hasa barani Afrika, mtoto ni tunu ya kipekee kwenye familia. Basi pia hata kwa familia ya Kazimoto na ukoo mzima ulikuwa na hamu kubwa ya kuona Sabina anapata mtoto. Hii tunaishuhudia ambapo msimulizi wa riwaya hii anapogusia jambo hili mwanzoni mwa sura ya kumi na moja, uk.159 – 160. Pia kama ilivyo nuizi ya riwaya hii suala kupoteza maisha kwa watu halipuuziwi kuelezwa pale linapobidi na kujitokeza. “ Tulinyamaza kwa muda. Halafu Tunza akaanza kunieleza juu ya watu ambao walikuwa wamekwisha kufa kijijini kwetu kwa muda wa miezi mine iliyopita.
“Wazee wote karibu wamekwenda. Ajabu ndiyo hiyo. Wazee wanafuatana, mmoja baada ya mwingine,” alisema. Wanapasuka tu kama kuni.”
Baada ya habari hizo za kifo kusimuliwa kwa Kazimoto, sasa mada iliyofuatia ni Tegemea kueleza nia iliyomleta kwa Kazimoto haikuwa kumwangalia Sabina na ujauzito, bali pia ni kumfuatilia mtoto wake Vumilia ambaye walipoteana na alikoelekea hawakuagana. Tegemea anamwuliza Kazimoto habari za Tegemea kama alishawahi kuzisikia kuwa yuko sehemu yo yote anayoifahamu. Kazimoto na Tegemea wanajadiliana na kuamua kwenda kumtafuta Vumilia ambaye maisha yake yalikuwa ya shida na taabu sana, miangaiko na mateso ya kila namana kama kwamba hakuwa na mzazi. Kuanzia uk, 161 hadi 175, tunasimuliwa namna Kazimoto na Tegemea walivyofuatilia na kufahamu anapoishi Vumilia ili mama yake aweze kumtoa kwenye hadha za dunia alizokuwa anakumbana nazo. Mwisho tunaona watu hawa, wanafanikiwa kumwona Vumilia lakini yeye anapinga kabisa kurudi kwa mama yake na kuamua kuendelea kuishi na mme wake, Moyokonde. Vumilia hakika aliridhia kuishi maisha ya taabu sana na mme wake baada ya kukataa kurudi nyumbani kwa mama yake. Hii ni ishara ya kumpenda Moyokonde hata kwa hali aliyokuwa nayo pia na kukubaliana na hali ya maisha yao. Ijapokuwa ilikuwa ni hali ngumu ambayo maisha ya wapendanao wawili hawa: wanaishi. Moyokonde ni mchoma mkaa ambaye kipato chake ni kidogo sana kulinganisha na mfumo wa gharama za maisha. Lakini pia haikuwa hali ngumu ya maisha tu, bali Vumilia alishakumbwa na matatizo ya kuvamiwa na vijana walitaka kumfanyia matendo ya ubakaji pamoja na kutaka kumuua, kama Moyokonde anavyomsimulia Kazimoto, uk. 172. Pia kabla ya hapo, Vumilia alikuwa akitajwa kuishi maisha ya shida sana; mfano, kufanya umalaya na kuangaika huko na huko, akitafuta kazi na pengine kufanya kazi za udangulo na kuuza baa.



SURA YA 12

Katika sura hii, ndipo tunapoona matatizo yanaikumba familia ya Kazimoto. Ni kipindi kigumu ambacho matumaini na matarajio ya kupata mtoto waliyemtegemea yalipofika mwisho, pale alipofariki dunia muda mfupi baada ya kuzaliwa kwa sababu ya kuwa na kichwa kikubwa ambacho, kilisababisha mtoto huyo kufa. Kazimoto alipatwa na butwaa hasa baada ya  kufikishwa wodini alipokuwa amelazwa mkewe, na kutaarifiwa ya kuwa mtoto wao amekatisha maisha baada ya kuzaliwa muda mfupi kama tunavyoona uk, 179. Kazimoto alikuwa na matumaini makubwa sana hasa kuhusu mtoto ila matumaini yake hayakuwa kama ilivyotarajiwa. Kwani alikuwa amekwisha anza kutayarisha mambo ambayo baadae yangekuwa matumizi katika malezi ya mtoto wao. Kazimoto aliona maisha hayana maana tena kwake, pia aliamua kusema ya kuwa Mungu hayupo: basi kama yupo ni mkatili. uk,180.



SURA YA 13

Kwa ufupi katika sura ya kumi na tatu, tunaona ya kuwa kutokana na matatizo yaliyowakumba wakina Kazimoto na mkewe, sasa wanaamua kutuliza mawazo. Waliamua kwenda kuwatembelea Manase na Salima hasa kipindi cha likizo ya mwezi Desemba. Walifanya hivyo. Walipanda basi na kwenda kwa Manase. Walipofika huko walikuta maisha kidogo yamebadilika tofauti na ilivyokuwa awali.  Manase hakuwa na gari lake, lilikuwa tayari limeharibika na kuchakaa. Mke wake Salima alikuwa amekonda kiasi kwamba ilikuwa vigumu kidogo kwa mtu aliyemwona miezi kadhaa iliyopita asingeweza kumtambua haraka. Walikaa kwa siku kadhaa na kuwajulia hali wenyeji wao kama ilivyokuwa dhima ya likizo hiyo hasa kwao.
Katika kuendelea kukaa nyumbani kwa Manase kama wageni waliowatembelea, ndugu zao: siku moja wapo kwenye meza ya chakula wanaendelea na kuweka kitu tumboni pia na mazungumzo; ghafla aliingia mtoto aliyekuwa na kichawa kikubwa sana. Alikuwa ni mtoto wa familia ya Manase. Kazimoto alimshangaa na kushutuka huku akiuliza kwa mshangao kuwa ni mtoto wa nani na kwa nini alikuwa hivyo. Jambo ambalo lilimkosesha amani Salima na kugutuka akikimbilia chumbani kwao kwa kilio kikubwa na kumshutumu Manase kwa kusababisha hatari hiyo. Manase alimjbu Kazimoto sababu ya mkewe kuwa vile. Kwamba aliposema maneno yale juu ya yule mtoto alimtonesha kidonda cha uchungu aliokuwa nao kuhusu mtoto huyo, kwani aliugua ugonjwa wa kichwa ambao chanzo chake ni Manase kuuchota kwa Pili aliyekuwa mpenzi wake wa zamani.
 Kazimoto pia alishutuka kwani tayari naye alikuwa ameisha wahi kutembea na pili. Pia mtoto wao alizaliwa kwa shida kwa sababu ya kuwa na kichawa kikubwa ambacho ndio ugonjwa huo. Baada ya Sabina kuyasikia maneano ya Manase na kuvuta kumbukumbu ya kifo cha mtoto wake: na pia kukumbuka barua ya Kazimoto aliyokuwa ameandikiwa na Pili, naye Sabina alianguka chini na kuzimia ghafla, uk,191 - 193. Maisha yalikuwa magumu kwao. Amani ilitoweka ndani ya nyumba kwa muda. Wanaume ndio waliokuwa chanzo cha upotevu wa amani hiyo.



SURA YA 14.
Hii ndio sura inayokamilisha kisa kinachozungumzwa katika riwaya hii. Ni sura ya mwisho ambayo kama ilivyo nadharia na mwono uliotumika kuandika kitabu hiki: mhusika mkuu Kazimoto anakata tamaa ya maisha hadi anafika hatua ya kujiua. Ndipo Kazimoto anapolinganisha maisha ya mtoto anayejifunza kutembea na maisha ya binadamu. Kazimoto anaona mtoto anajaribu kutembea halafu anashindwa na kuanguka chini. Hali hii anafananisha na maisha ya mtu aliyefanya mambo mengi duniani alafu baadae anashindwa kitu kidogo na matumaini yake yanaishia hapo ama maisha ya mwanadamu na kifo chake, uk,194.
Baada ya mawazo hayo, Kazimoto alihojiana na mkewe kama ifuatavyo:
“Mke wangu,” nilimwita.
“Bwana’ngu,”aliitikia.
“Sijui kwa nini ninaishi.”
“Nimechoka na maswali yako ya kijinga.” Alisema.
“Huwezi kuishi kama watu wengine? Wewe nani?”
“Mimi sijijui,” nilimwabia.
“Hakika sikufahamu kwamba wewe ni kichwamaji namna hiii! Sikufahamu!” Alilia, machozi yakamtoka. Kwa muda mfupi machozi yake yalikuwa mekundu. Alikwenda kulala . . .”
Baada ya hapo Kazimoto utamaushi ulikuwa tayari umemzidi nguvu, hadi anaamua kujiondoa duniani, kama anavyonena; . . .nilikwenda ndani ya chumba cha kulala. Sabina alikuwa amejifunika shuka akilia kwa kwikwi. Nilichukua kitu fulani. Nilikuwa sifahamu jambo nililokuwa ninafanya, isipokuwa nguvu Fulani zilizokuwa zikiniongoza – sauti! Sauti! . . . Sabina alipoamka, ndugu zangu, kwa kusikia mlio wa bunduki, alimkuta mumewe amelala chini karibu na meza, kichwa chake kikivuja damu, bastola pembeni. Alipotazama juu ya meza aliona kijikaratasi kidogo kilichokuwa kimeandikwa manenao haya:
     Nimejiua, siwezi kuendelea kuzaa kizazi kibaya. Pia sikuona tofauti kati yangu na mdudu au mnyama. Akili! Akili! Akili ni nini? Pia nikiwa duniani sikuwahi kupata kukutana hata siku moja na mtu anayeamini kwamba kuna Mungu. Watu anaogopa kufa na kwenda motoni hao nimewaona, tena wengi sana. Mtu ye yote asilaumiwe kwa kifo changu. Mimi kabla ya kufa ninaungama mbele ya ulimwengu kwamba nilimwua ndugu yangu ingawa sikumgusa, uk,194 - 196. Huo ndio ulikuwa mwisho wa maisha ya Kazimoto na mwisho wa riwaya hii.
Lakini mwisho wa kitabu hiki kinamsifia mhusika kama jasiri na mkombozi wa maisha ya Afrika. Na pengine kuona kuwa kifo sio suluhisho la matatizo katika maisha: na hivyo mbinu sahihi ni kupambambana matatizo hayo kwa kutafuta mbinu sahihi za kuyatatua, uk, 196.





10 comments: