DHANA YA UDHANAISHI
Katika kuelezea
nadharia hii tutajikita kwanza kuangalia maana ya udhanaishi kwa mujibu wa
wataalam mbalimbali, waasisi wake kisha mihimili yake na mwisho tutamalizia na
uchambuzi wa Riwaya ya “Kichwamaji” kwa kutumia nadharia hii.
MAANA
YA UDHANAISHI
Wataalam mbalimbali
wameeleza maana ya udhaishi kama vile;
Kimani Njogu na Rocha Chimerah (1999) wanasema
“Udhanaishi ni nadharia inayojishughulisha zaidi na dhana ya Maisha” swali la
kimsingi katika nadharia hii ni ; Maisha ni nini?. Wadhanaishi huchunguza kwa undani nafasi ya mwanadamu ulimwenguni, pia
wanajishughulisha na uchunguzi kuhusu
uhuisiano uliopo kati ya binadamu na Mungu.
Wamitila, K. W. (2003)
Katika Kamusi ya fasihi Istilahi na nadharia amefafanua “Udhanaishi ni dhana
inayotumiwa kuelezea falsafa ya kuwako na Maisha. Dhana hii inatumiwa kueleza
Maono au Mitazamo unaohusiana na hali ya Maisha ya binadamu, nafasi na jukumu
lake ulimwenguni na uhusiano wake (au kutokuwepo kwake) na Mungu.
Wanjala Simiyu (2012) katika Kitovu cha fasihi
simulizi “Udhanaishi ni falsafa au Mtazamo wa Maisha ulio na kitovu chake
katika swali kuwa, Maisha ni nini na yana maana gani kwa binadamu?, ni kwa njia
gani mwanadamu anaweza kuyabadilisha
maisha yake yaliyojaa dhiki, mashaka na huzuni.
WAASISI
WA UDHANAISHI
Udhanaishi unahusishwa
kwa kiasi kikubwa na Mwana theolojia wa
Ki-Den Soren Kier Kegaard, mwanafalsafa wa Kijerumani Friedrich
Nietzsche na wengine kama Martin Heidegger na Gabriel Marcel. Na baadae baada
ya vita kuu za dunia (1 & 2) muasisi mkuu wa nadharia hii alikuwa Jean Paul
Satre na katika Fasihi ya Kiswahili muasisi wa nadharia hii ni mdhanaishi E.
Kezilahabi.
E. Kezilahabi ni mmoja kati ya wadhanaishi
ambapo riwaya zake mfano; Kichwamaji, Rosa Mistika & Dunia uwanja wa fujo amejikita
katika nadharia ya Udhanaishi.
MIHIMILI
YA UDHANAISHI
Waandishi mbalimbali
wameweza kutoa mihimili ya udhanaishi, kwa kuwarejelea Wafula R. M & Kiman Njogu
(2007) wao wameiainisha mihimili hiyo kama ifuatavyo;
·
Wanatilia mkazo matatizo halisi yanayomsibu
mwanadamu na wanakwepa imani ya kinjozi juu ya imani ya kuishi.
·
Hawaamini uwepo wa Mungu na uumbaji wake
wa ulimwengu.
·
Juhudi za mtu binafsi kujisaka au
kupambana na maisha huishia katika ukengeushi na hatimaye hukutwa na umauti.
·
Maudhui yanayotajwa na wadhanaishi ni
kama vile uhuru wa mtu binafsi, uwezo wake wa kujifikiria na kujiamlia mambo.
·
Hujadili hali kama vile mashaka na
uchovu wa mambo mbalimbali yanayotutatiza maishani na jinsi yanavyoathiri
maisha ya Binadamu.
·
Pia hujadili maudhui ya ukengeushi (hali
ya kukatatama au kutokuwa na uhakika).
NADHARIA
YA UDHANAISHI KATIKA RIWAYA YA KICHWAMAJI
Kichwamaji ni Riwaya ya
E. Kezilahabi iliyojikita zaidi katika nadharia ya udhanaishi, kwa kutumia
riwaya hii tunajadili jinsi nadharia hii ilivyojitokeza kama ifuatavyo;
Katika udhanaishi Waandishi
wanatilia mkazo matatizo halisi yanayomsibu mwanadamu, wanakwepa imani ya
Kinjozi juu ya maana ya kuishi, wanakwepa kutueleza ni kwanini mtu azaliwe,
ateseke kisha afe. Riwaya
ya Kichwa Maji mwandishi E.Kezilahabi amewachora wahusika kama Kazimoto aliyepatwa na matatizo ya ugonjwa wa kifua kikuu na
kupelekea kutoendelea na masomo
imedhihirishwa katika ukurasa wa (10) na
baada ya kupona alipotaka kuendelea na masomo akakosa pesa ya kulipia ada na
hivyo akaanza kutafuta kazi ya muda ili apate hela ya kulipa ada, hii nayo pia
imejitokeza katika ukurasa wa 10.
Kwao Mungu yupo au
aliumba ulimwengu ni suala ambalo hawalishughulikii kwasababu halioani na
mantiki ya fikra zao. Pia E.Kezilahabi amemchora mhusika Kazimoto kwamba hamuamini
Mungu pale alipokuwa akibishana na wazee walipokuwa wakinywa pombe wakati
alipoenda kumtembelea Kamata, ukurasa wa (51), pia katika ukurasa wa (121)
walipokuwa katika maongezi kati Manase, Kazimoto na Salima. Pia katika ukurasa
wa (180) Kazimoto haamini uwepo wa Mungu baada ya kufiwa na mtoto wake alisema
“ Kama kweli Mungu alikuwepo sikuweza kuona kwanini aliweza kufanya ukatili
mkubwa kama huo”.
Maudhui yanayotajwa
kama uhuru wa mtu binafsi, uwezo wa mtu kujifikiria na kujiamulia na pia wajibu
wa binadamu katika ulimwengu. Mwandishi E. Kezilahabi amemchora muhusika
Kazimoto alipokuwa akitaka uhuru wa kujiamlia mfano pale alipoondoka bila ya
kuaga na kwenda kumtembelea Kamata na
baada ya kurudi mama yake alimuuliza alikwenda wapi katika ukurasa wa (64),
akajibu “Mapenzi ya kitoto namna hiyo mimi siyapendi kila siku niondokapo
nyumbani unaniuliza ninakwenda wapi.” Pia Manase alikuwa analikuwa anajiamulia
kuchagua mwanamke anayempenda pale alipojibu barua kwa wazazi wake kuwa tayari
ana mwanamke anayetaka kumuoa na siye
Rukia, katika ukurasa wa (26).
Maudhui ya Ukengeushi,
hali ya kutokuwa na uhakika na hali ya kukata tamaa. Mwandishi E.Kezilahabi
amemchora muhusika Rukia aliyekata tamaa ya maisha baada ya kupata ujauzito
katika ukurasa wa (83) ambapo Kazimoto anaambiwa “ Ndugu yako amekufa
akikulilia na aliomba umsamehe na amekuomba usisikitike sana hata yeye alikuwa
haoni tena maana ya kuishi”. Pia Kazimoto alikata tamaa ya kuishi baada ya
mtoto wake kufariki tunaona katika ukurasa wa (180) anasema “ Mimi siwezi
kuishi tena”.
Juhudi za mtu kujisaka ili aweze
kujielewa maishani, huvunjika na pia huishia katika mauti. Mfano katika kitabu
cha kichwa maji mwandishi E. Kezilahabi amemchora mhusika Kazimoto aliyekuwa na
juhudi za kumsomesha Rukia lakini baadae akaishia kupata ujauzito na kupelekea
kukatisha masomo,hatimaye kupelekea hadi kifo chake, ukurasa wa (18). Pia
Kazimoto na mkewe walikuwa na juhudi za kupata mtoto lakini juhudi hizo
hazikufanikiwa kwani Sabina wakati wa kujifungua mtoto alifariki, katika
ukurasa wa (180).
Udhanaishi unajadili hali kama vile Mashaka na
Uchovu wa mambo mbalimbali yanayotutatiza maishani na jinsi yanavyoathiri
maisha ya binadamu. Mfano mwandishi E.
kezilahabi katika kitabu chake cha Kichwa maji anaonesha mashaka katika familia
ya Mzee Mafuru kutokana na mambo ya
kishirikina na ambayo yalikuwa yakifanyika wakati wa usiku katika ukurasa wa (24)
, mama yake Kazimoto alipokuwa akimwambia Kazimoto “ Hujafahamu kwamba sisi
sote maisha yetu yapo hatarini
Hivyo basi E.Kezilahabi katika maandishi (kazi
zake za kifasihi) anaonekana kwamba yu miongoni mwa wadhanaishi wasiokuwa na
uhakika kwamba Mungu yupo.
MAREJELEO
Njogu, K. na Chimerah,
R. (1999): Ufundishaji wa fasihi, nadharia na mbinu, Jomo Kenyata Foundation
Nairobi.
Kezilahabi, E. (2008):
Kichwa Maji, Vide-Muwa Publishers.Nairobi.
Wafula, R.N. na Njogu,
K. (2007): Nadharia za uhakiki wa fasihi, Sai Industries limited. Nairobi.
Wamitila, K.W. (2003):
Kamusi ya fasihi Istilahi na nadharia. Focus Publications limited. Nairobi
Kenya
No comments:
Post a Comment