Kwa mujibu wa Senkoro, F.M.K (1987), Uhalisia
wa kijamaa ni hatua ya juu ya
uhalisia wa kihakiki. Ni uhalisia ambao msingi wake mmojawapo mkuu ni wa
harakati za kitabaka. Harakati hizi katika uhalisia huu huonyeshwa katika
uhalisia wake wote bila kuficha jambo lolote lile.
Kwa mujibu wa Njogu, K na Wafula R.M (2007), Uhalisia
wa kijamaa ni mbinu ya utunzi na uhakiki inayomzingatia binadamu kama uti
wa mgongo wa kuwepo kwa ulimwengu na maana ya ulimwengu ule. Waundaji wa
nadharia hii wameathiriwa na mtazamo wa Kimaksi kuhusu ulimwengu na historia.
Maxim Gorki mmojawapo wa waasisi wa uhalisia wa kijamaa, anasema kwamba mambo
yote mazuri yanayotamanika ulimwenguni yameumbwa au kuelezwa na binadamu.
Kwa mujibu wa Wamitila, K.W (2003), Uhalisia wa
kijamaa ni mtazamo ambao hujaribu kusisitiza uwasilishi wa uhalisia
unaotilia mkazo mkubwa maendeleo ya kihistoria yanayokiuka ubepari na kufikia
usoshalisti. Kazi za kifasihi ambazo zimeandikwa katika misingi ya uhalisia
hupaswa kulenga kuwafikia wasomaji wa kawaida.
Vigezo vya uhalisia wa kijamaa
Huonyesha uhalisia wake kwa uelekeo wa kijamaa. Uhalisia wa kijamaa
huonyesha mambo katika misingi ya kijamaa kwa namna ya kupinga matabaka hivyo
njia ya uzalishaji mali humilikiwa kwa usawa.
Huwa na muundo fulani wa
kihistoria ambao huonekana kama mvutano kati ya matabaka. Ili jamii iwe na
mabadiliko au maendeleo lazima iwe na historia fulani kwa kutoka katika hatua
moja kwenda nyingine. Mfano Karl Marxy na Fredrick walisema “jamii zote
ulimwenguni ilibidi zipitie katika hatua ya ukatili umwinyi ubwanyenye ukabaila ubepari
ujamaa, ili jamii iweze
kufikia usawa na hivyo kuleta maendeleo katika jamii.
Kusisitiza kuwa maisha ni matendo na kwa ubunifu ambao nia yake ni
kuonyeresha ukuaji wa binadamu na kuweza kuibuka mshindi katika mapambano ya
nguvu za kiasili. Lengo kubwa la nadharia hii
ni kuonyesha namna waandishi wanavyowatumia wahusika mbalimbali katika
jamii wanavyotakiwa kuwa watu wenye ujuzi na mbinu mbalimbali za kuweza
kupambana na matatizo yanayowakumba katika jamii, mfano masuala ya unyonyaji,
rushwa, matabaka na umaskini, ili mwisho wake waweze kuyashinda matatizo hayo.
Chanzo kikuu cha mivutano ni uzalishaji mali. Hii hutokea pale ambapo
tabaka la chini linapojaribu kupambana na tabaka la juu ili kuweza kumiliki
nyenzo mbalimbali za uzalishaji mali kama vile mashamba na viwanda, hali ambayo
hupelekea tabaka la chini kupata usawa katika jamii.
Fasihi huchukuliwa kama silaha ya kupinga dhuluma, unyonyaji na uonevu.
Tunaona kuwa waandishi wengi wa fasihi huandika kazi zao kwa lengo la
kulikomboa tabaka la chini kutoka kwenye mikono ya dhuluma, unyonyaji na uonevu
ili kuweza kuleta usawa katika tabaka hilo tawaliwa kwenye nyanja zote za
maisha yaani; kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi.
Hulenga maisha ya baadaye na
ujenzi wa jamii mpya yenye raha na ufanisi. Uhalisia wa kijamaa hupigania jamii
yake kuachana na mambo yanayokwamisha maendeleo katika jamii husika kwa
kuwachora wahusika wanaopigana kuleta mabadiliko katika nyanja zote yaani
kifikra, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni ili wawe na jamii moja yenye raha na ufanisi.
Huamini baada ya wafanyakazi wa viwandani kuchukua silaha na kupigania
haki yao dhidi ya mwajiri ambaye daima ni mnyonyaji wa nguvu zao, hali hii
husababisha mapinduzi ambayo huzaa jamii isiyo na matabaka. Kazi nyingi za
uhalisia wa kijamaa huamini kuwa suluhisho la unyonyaji wa tabaka la chini ni
tabaka hili (wanyonge ambao ndio wafanyakazi wa tabaka lenye nguvu) kupambana
na tabaka tawala kwa kutumia silaha ili kuzipigania haki zao kwa kupambana na
wanyonyaji, wanauhalisia wa ujamaa wanaamini kuwa kutapelekea mapinduzi katika
jamii husika hivyo kuzaliwa kwa jamii
mpya isiyo na matabaka wala unyonyaji na hatimaye jamii kuishi katika misingi
ya usawa.
Riwaya
ya Nyota ya Rehema iliyoandikwa na Mohamed Suleiman ni riwaya ya uhalisia wa
kijamaa kulingana na maudhui yake kama ifuatavyo:
Uhalisia wa kijamaa huwa na muundo fulani wa kihistoria ambao huonekana
kama mvutano kati ya matabaka ambao chanzo kikuu cha mivutano hiyo ni
uzalishaji mali. Kwa kutumia riwaya ya Nyota ya Rehema, mwandishi
Mohamed Suleiman ameonyesha muundo wa Umwinyi ambao wachache wanahodhi mashamba
na mazao na kuwaweka maskini kuyalima na kulipia kodi kwa kuwafanyia kazi na
kuwapatia sehemu ya mazao wanayozalisha, ambapo vitendo hivyo husababisha
mivutano baina ya tabaka tawala na tawaliwa. Mfano, kulitokea mivutano kati ya Karimu na Rehema pale ambapo Karimu
alidiriki kumpeleka Rehema kwa mwanasheria Bwana Mudir kwa nia ya kumdhulumu
urithi wa shamba na nyumba katika eneo la Ramwe ambalo Bwana Fuad alimpa Rehema
lakini bila kumpatia hati miliki. Na
baada ya kifo cha Fuad ndipo Rehema aliponyang’anywa urithi huo baada ya Karim
kutengeneza hati za kugushi na kumlazimisha Rehema kuweka sahihi kwa kidole
chake. Mfano Rehema alisema,
“Konde zilizomo na shamba lenyewe ni mali yangu
Bwana Mudir na mimi ndiye mtoto wa marehemu Bwana Fuad … Baba Fuad Salum” Yule
kijana alitaharuki sikumbuki Bwana Mudir alipayuka kijana mkakamavu kwa sauti
yenye kulipa kila neno uzito wake kuwa al-marhum kaacha zaidi ya watoto wawili,
mmoja ni Samiri ambaye yupo Ulaya anamaliza masomo yake, wa pili ni Ahli wa
Bwana Mudir wa jimbo la mjini (mke wa Karim). (uk.143)
Hivyo kutokana na unyonyaji uliofanywa na tabaka
tawala ilipelekea kutokea kwa mapinduzi ambayo yalileta mabadiliko makubwa
katika jamii hiyo na hivyo kukawa na usawa katika umilikaji na uzalishaji mali.
Uhalisia wa kijamaa hulenga maisha ya baadaye na ujenzi wa jamii mpya
yenye raha na ufanisi. Katika riwaya ya Nyota ya Rehema mwandishi
amemtumia mhusika Rehema aliyekuwa anajaribu kupigania haki yake ili apate
urithi na aje kuishi maisha ya raha na ufanisi, pia Sulubu ambaye alidiriki
hata kumuua Karim alipelekwa gerezani, tendo hili liliwafanya wananchi
wakaandamana na kupinga unyanyasaji na kufanya mapinduzi dhidi ya utawala wa
kimwinyi, ili waweze kujenga jamii mpya isiyo na matabaka. Mfano mwandishi
anasema,
“Poeni wananchi! poeni wananchi! Dhuluma imeshapinduliwa! Haki
tupu! Uhuru na haki …!” "Hekaheka
za mapinduzi zilipomalizika Rehema, Sulubu na mtoto wao wanarejea katika shamba
lao la pakani na kuendelea kuamrisha … ” (uk. 168)
Hivyo inadhihirika katika riwaya hii kuwa uhalisia
wa kijamaa huwa na lengo la kujenga jamii mpya yenye maendeleo, kwani juhudi
zote huwa ni kwa ajili ya kupinga
dhuluma na kuleta jamii yenye raha na ufanisi.
Uhalisia wa kijamaa huonyesha uhalisi wake kwa uelekeo wa kijamaa.
Katika riwaya ya Nyota ya Rehema imeonyesha sana maudhui yake
kuwa ya uhalisia wa kijamaa mfano kwa kurejelea wahusika kama Kidawa, Chiku,
Rehema na Ruzuna wameonyesha kuishi maisha ya kijamaa (uk.43-44). Vilevile Bi
Kiza na mzee Juma nao upendo wao kwa Rehema unaonyesha ujamaa na pia kitendo
cha wananchi wa tabaka la chini kuungana kumtetea Sulubu pale alipokamatwa baada ya kumuua Karim, umoja huo ulionyesha
ujamaa wao kupambana na serikali hatimaye wakafanya mapinduzi ya utawala
uliokuwa madarakani (uk.168)
“sauti za wanyonge moja ikiamsha nyingine,
zilivuma na kushinikiza Mtoeni Sulubu! Mtoeni Sulubu! Mtoeni Sulubu! … ”
Hivyo katika riwaya hii ya Nyota ya Rehema
imeonyesha wazi suala la uelekeo wa uhalisia wa kijamaa.
Uhalisia wa kijamaa huchukuliwa kama silaha ya kupinga dhuluma,
unyonyaji na uonevu. Maudhui katika riwaya hii ya Nyota ya Rehema yameonyesha
uhalisia wa kijamaa kwa kupinga dhuluma, unyonyaji na uonevu kama inavyoonekana
katika (uk.168) ambapo wananchi wa tabaka la chini wanaungana katika kupinga
dhuluma na unyanyasaji uliokuwa unafanywa na serikali juu yao baada ya kufungwa
kwa Sulubu, pia katika (uk.80-82) tunamuona Bi Kiza akipigania haki ya Rehema
binti yake Fuad katika kutafuta urithi wa kiwanja alichoacha mama yake Aziza
baada ya kifo chake. Bi Kiza anasema, “nimekuja kukuchukua”
“Ukadai haki zako”
Marehemu mama yako … kaacha vitu
chungu nzima Ramwe …”
kadhalika (uk. 167-168) Sulubu alifikia kumcharanga
mapanga Karim aliyetaka kuwadhulumu eneo la shamba lao. Mwandishi anasema,
“Sura aliyoiona ilikuwa ya kiwiliwili cha Karim
kimeanguka kifudifudi, vipande viwili …” Hivyo mwandishi wa riwaya hii ameonyesha jinsi
uhalisia wa kijamaa unavyochukuliwa kama silaha ya kupinga dhuluma, unyonyaji
na uonevu katika jamii.
Uhalisia wa kijamaa huamini baada ya wafanyakazi wa viwandani kuchukua
silaha na kupigania haki yao dhidi ya mwajiri wao ambaye daima ni mnyonyaji wa
nguvu zao, hali hii husababisha mapinduzi ambayo huzaa jamii isiyo na matabaka.
Katika riwaya ya Nyota ya Rehema mwandishi amamtumia mhusika Sulubu ambaye alikuwa mme wa Rehema katika
kutetea haki za wanyonge. Suala hili la utetezi wa haki za wanyonge ilipelekea
Sulubu kuhukumiwa kunyongwa kwa kosa la kumuua Karim ambaye alitaka
kumnyang’anya shamba lakini wananchi wengine wakashirikiana na wanajeshi
kupinga suala hilo na hatimaye kukafanyika mapinduzi, mfano mwandishi
anaposema,
“Ndipo ambapo vizazi vya wanyonge vilivyokuwa
jeshini vilipounda nguvu kwa siri na kufanya mapinduzi yaliyofanikiwa muda
mfupi na kabla Sulubu kunyongwa (uk.168).
Hapa ndipo tunaona wanajeshi wanaipindua serikali
yao na wananchi wanakuwa huru na kuondokana na suala la matabaka na kuishi
kijamaa.
Uhalisia wa kijamaa husisitiza kuwa maisha
ni matendo na ubunifu ambao nia yake ni kuonyesha ukuaji wa binadamu na kuweza
kuibuka mshindi katika mapambano ya nguvu za kiasili. Katika riwaya hii ya Nyota
ya Rehema mwandishi amewatumia wahusika Rehema na Sulubu ambao maisha
yao yameelezwa kiuyakinifu. Kwanza maisha ya Rehema yanaonyeshwa tangu
alipozaliwa kisha kukataliwa na baba yake hatimaye akatoroka kwenda mjini na
kukumbana na misukosuko mingi na anaamua kurudi kijijini kwa baba yake kuomba
msamaha. Lakini baada ya kukumbwa na yote haya Rehema anaamua kuolewa na Sulubu
ambaye alikuwa mtu mwema na mchapa kazi. Wakiwa pamoja Rehema na Sulubu
waliendelea kupatwa na misukosuko hatimaye wanaibuka kuwa washindi. Pia tunaona
Rehema na Sulubu walionekana kuwa wabunifu pale ambapo walihamia kwenye shamba
lisilokuwa na rutuba baada ya kunyang’anywa shamba lao la urithi. Rehema na
Sulubu wanaamua kuwachoma na kuwasagasaga wadudu ili kurutubisha shamba lao.
Mfano mwandishi anasema,
Njia
rahisi ya mwisho aliyoiona Rehema
ilikuwakuwa sagasaga sangara, konokono na jongoo ili kuwageuza mbolea … ”
(uk. 154)
Hivyo basi Mohamed S. Mohamed ameonyesha jinsi
tabaka la chini linavyokuwa na ubunifu ili kuweza kuibuka na ushindi dhidi ya
tabaka tawala katika kuleta usawa katika jamii.
Uhalisia wa kijamaa huonyesha kuwa chanzo kikuu cha mivutano ni
uzalishaji mali. Katika riwaya ya Nyota ya Rehema mwandishi
anaonyesha jinsi au namna suala la ardhi kama chanzo cha uzalishaji mali
linavyoleta migogoro katika jamii. Kwa kudhihirisha hilo mwandishi amewatumia
wahusika kama Rehema na Sulubu ambao walikuwa na mgogoro au mvutano na Karim
kuhusu shamba la urithi alilopewa Rehema. Mwandishi anaowanyesha Karim na mke
wake wakipingana juu ya wazo la kwenda kumdhulumu Rehema shamba lake ambalo
alipewa na baba yake kama urithi. Mfano Salma anasema,
“Karim! Haiwezekani! Shamba lile walipewa na
marehemu baba mwenyewe” (uk.164)
Mgogoro mwingine ni wa Karim kutaka kudhulumu
shamba la Rehema na mumewe, suala hilo lilipelekea kifo cha Karim ambaye aliuawa na Sulubu mme wa Rehema. Mfano Rehema
anasema,
“Sura
niliyoiona ilikuwa ya kiwiliwili cha Karim kimeanguka kifudifudi vipande
viwili…” (uk.168).
Pia tunaona mvutano mwingine ni kati ya tabaka
tawala na tabaka tawaliwa (chini) mvutano huu unatokana na kufungwa kwa Sulubu
ambapo wananchi wanaungana na kupinga serikali yao hatimaye mapinduzi
yakatokea. Mfano mwandishi anasema,
“Sauti za
wanyonge moja ikiamsha nyingine zilivuma na kushinikiza, Mtoeni Sulubu! Mtoeni
Sulubu!” (uk.168)
mwandishi
ametumia migogoro hii ili kuonyesha mapinduzi yenye kuleta usawa katika jamii.
Kwa ujumla mwandishi wa riwaya ya Nyota ya Rehema ya
mwandishi Mohamed S. Mohamed amejaribu kuonyesha namna/jinsi usawa unavyoweza
kupatikana katika jamii. Suala hili la usawa katika jamii isiyokuwa na matabaka
Mohamed amejaribu kuonyesha namna suluhisho linavyoweza kupatikana kuwa kuwa ni
tabaka la chini kuweza kufanya mapinduzi kama harakati za kimapinduzi
zilizokuwa zikifanywa na wahusika kama Sulubu Rehema pia hata Wanajeshi. Hata hivyo
katika jamii ya sasa uhalisia wa kijamaa unaonekana kushindwa kutekelezwa
katika jamii kutokana na nguvu za mfumo
wa kibepari unaonekana kuitawala dunia na watu wake kwa ujumla.
MAREJELEO:
Masebo J.A and Nyangwine N, (2002) Nadharia ya
Fasihi. Dar es Salaam: Afroplus Industries Ltd.
Mazrui A
and Syambo B (1992) Uchambuzi wa Fasihi. Nairobi: East African
Educational Publishers
Mohamed S.M (1976), Nyota ya Rehema.
Nairobi: Oxford University Press East Africa Ltd.
Njogu K & Wafula R.M (2007) Nadharia za
Uhakiki wa Fasihi. Kenya: The Jomo Kenyatta Foundation.
Senkoro F.E.M.K (1987) Fasihi na Jamii. Dar
es Salaam: Press and Publishing Centre.
Wamitila K.W (2003) Fasihi, Istilahi na
Nadharia. Kenya: Focus Books.
FOR MORE INFO CALL 0768607147/0679607147
FOR MORE INFO CALL 0768607147/0679607147
Nimesaidika Asante,
ReplyDeleteNashukuru
ReplyDelete