Thursday, July 14, 2016

UDHANAISHI



 DHANA YA UDHANAISHI
Katika kuelezea nadharia hii tutajikita kwanza kuangalia maana ya udhanaishi kwa mujibu wa wataalam mbalimbali, waasisi wake kisha mihimili yake na mwisho tutamalizia na uchambuzi wa Riwaya ya “Kichwamaji” kwa kutumia nadharia hii.
MAANA YA UDHANAISHI
Wataalam mbalimbali wameeleza maana ya udhaishi kama vile;
 Kimani Njogu na Rocha Chimerah (1999) wanasema “Udhanaishi ni nadharia inayojishughulisha zaidi na dhana ya Maisha” swali la kimsingi katika nadharia hii ni ; Maisha ni nini?. Wadhanaishi  huchunguza kwa undani  nafasi ya mwanadamu ulimwenguni, pia wanajishughulisha na uchunguzi kuhusu  uhuisiano uliopo kati ya binadamu na Mungu.
Wamitila, K. W. (2003) Katika Kamusi ya fasihi Istilahi na nadharia amefafanua “Udhanaishi ni dhana inayotumiwa kuelezea falsafa ya kuwako na Maisha. Dhana hii inatumiwa kueleza Maono au Mitazamo unaohusiana na hali ya Maisha ya binadamu, nafasi na jukumu lake ulimwenguni na uhusiano wake (au kutokuwepo kwake) na Mungu.
 Wanjala Simiyu (2012) katika Kitovu cha fasihi simulizi “Udhanaishi ni falsafa au Mtazamo wa Maisha ulio na kitovu chake katika swali kuwa, Maisha ni nini na yana maana gani kwa binadamu?, ni kwa njia gani mwanadamu  anaweza kuyabadilisha maisha yake yaliyojaa dhiki, mashaka na huzuni.
WAASISI WA UDHANAISHI
Udhanaishi unahusishwa kwa kiasi kikubwa na Mwana theolojia wa  Ki-Den Soren Kier Kegaard, mwanafalsafa wa Kijerumani Friedrich Nietzsche na wengine kama Martin Heidegger na Gabriel Marcel. Na baadae baada ya vita kuu za dunia (1 & 2) muasisi mkuu wa nadharia hii alikuwa Jean Paul Satre na katika Fasihi ya Kiswahili muasisi wa nadharia hii ni mdhanaishi E. Kezilahabi.
 E. Kezilahabi ni mmoja kati ya wadhanaishi ambapo riwaya zake mfano; Kichwamaji, Rosa Mistika & Dunia uwanja wa fujo amejikita katika nadharia ya Udhanaishi.
MIHIMILI YA UDHANAISHI
Waandishi mbalimbali wameweza kutoa mihimili ya udhanaishi, kwa kuwarejelea Wafula R. M & Kiman Njogu (2007) wao wameiainisha mihimili hiyo kama ifuatavyo;
·         Wanatilia mkazo matatizo halisi yanayomsibu mwanadamu na wanakwepa imani ya kinjozi juu ya imani ya kuishi.
·         Hawaamini uwepo wa Mungu na uumbaji wake wa ulimwengu.
·         Juhudi za mtu binafsi kujisaka au kupambana na maisha huishia katika ukengeushi na hatimaye hukutwa na umauti.
·         Maudhui yanayotajwa na wadhanaishi ni kama vile uhuru wa mtu binafsi, uwezo wake wa kujifikiria na kujiamlia mambo.
·         Hujadili hali kama vile mashaka na uchovu wa mambo mbalimbali yanayotutatiza maishani na jinsi yanavyoathiri maisha ya Binadamu.
·         Pia hujadili maudhui ya ukengeushi (hali ya kukatatama au kutokuwa na uhakika).
NADHARIA YA UDHANAISHI KATIKA RIWAYA YA KICHWAMAJI
Kichwamaji ni Riwaya ya E. Kezilahabi iliyojikita zaidi katika nadharia ya udhanaishi, kwa kutumia riwaya hii tunajadili jinsi nadharia hii ilivyojitokeza kama ifuatavyo;
Katika udhanaishi Waandishi wanatilia mkazo matatizo halisi yanayomsibu mwanadamu, wanakwepa imani ya Kinjozi juu ya maana ya kuishi, wanakwepa kutueleza ni kwanini mtu azaliwe, ateseke kisha afe. Riwaya  ya Kichwa Maji mwandishi E.Kezilahabi amewachora wahusika kama  Kazimoto aliyepatwa  na matatizo ya ugonjwa wa kifua kikuu na kupelekea  kutoendelea na masomo imedhihirishwa  katika ukurasa wa (10) na baada ya kupona alipotaka kuendelea na masomo akakosa pesa ya kulipia ada na hivyo akaanza kutafuta kazi ya muda ili apate hela ya kulipa ada, hii nayo pia imejitokeza katika ukurasa wa 10.
Kwao Mungu yupo au aliumba ulimwengu ni suala ambalo hawalishughulikii kwasababu halioani na mantiki ya fikra zao. Pia E.Kezilahabi amemchora mhusika Kazimoto kwamba hamuamini Mungu pale alipokuwa akibishana na wazee walipokuwa wakinywa pombe wakati alipoenda kumtembelea Kamata, ukurasa wa (51), pia katika ukurasa wa (121) walipokuwa katika maongezi kati Manase, Kazimoto na Salima. Pia katika ukurasa wa (180) Kazimoto haamini uwepo wa Mungu baada ya kufiwa na mtoto wake alisema “ Kama kweli Mungu alikuwepo sikuweza kuona kwanini aliweza kufanya ukatili mkubwa kama huo”.
Maudhui yanayotajwa kama uhuru wa mtu binafsi, uwezo wa mtu kujifikiria na kujiamulia na pia wajibu wa binadamu katika ulimwengu. Mwandishi E. Kezilahabi amemchora muhusika Kazimoto alipokuwa akitaka uhuru wa kujiamlia mfano pale alipoondoka bila ya kuaga na  kwenda kumtembelea Kamata na baada ya kurudi mama yake alimuuliza alikwenda wapi katika ukurasa wa (64), akajibu “Mapenzi ya kitoto namna hiyo mimi siyapendi kila siku niondokapo nyumbani unaniuliza ninakwenda wapi.” Pia Manase alikuwa analikuwa anajiamulia kuchagua mwanamke anayempenda pale alipojibu barua kwa wazazi wake kuwa tayari ana mwanamke anayetaka  kumuoa na siye Rukia, katika ukurasa wa (26).
Maudhui ya Ukengeushi, hali ya kutokuwa na uhakika na hali ya kukata tamaa. Mwandishi E.Kezilahabi amemchora muhusika Rukia aliyekata tamaa ya maisha baada ya kupata ujauzito katika ukurasa wa (83) ambapo Kazimoto anaambiwa “ Ndugu yako amekufa akikulilia na aliomba umsamehe na amekuomba usisikitike sana hata yeye alikuwa haoni tena maana ya kuishi”. Pia Kazimoto alikata tamaa ya kuishi baada ya mtoto wake kufariki tunaona katika ukurasa wa (180) anasema “ Mimi siwezi kuishi tena”.
        Juhudi za mtu kujisaka ili aweze kujielewa maishani, huvunjika na pia huishia katika mauti. Mfano katika kitabu cha kichwa maji mwandishi E. Kezilahabi amemchora mhusika Kazimoto aliyekuwa na juhudi za kumsomesha Rukia lakini baadae akaishia kupata ujauzito na kupelekea kukatisha masomo,hatimaye kupelekea hadi kifo chake, ukurasa wa (18). Pia Kazimoto na mkewe walikuwa na juhudi za kupata mtoto lakini juhudi hizo hazikufanikiwa kwani Sabina wakati wa kujifungua mtoto alifariki, katika ukurasa  wa (180).
 Udhanaishi unajadili hali kama vile Mashaka na Uchovu wa mambo mbalimbali yanayotutatiza maishani na jinsi yanavyoathiri maisha ya binadamu. Mfano mwandishi  E. kezilahabi katika kitabu chake cha Kichwa maji anaonesha mashaka katika familia ya Mzee Mafuru  kutokana na mambo ya kishirikina na ambayo yalikuwa yakifanyika wakati wa usiku katika ukurasa wa (24) , mama yake Kazimoto alipokuwa akimwambia Kazimoto “ Hujafahamu kwamba sisi sote maisha yetu yapo hatarini
 Hivyo basi E.Kezilahabi katika maandishi (kazi zake za kifasihi) anaonekana kwamba yu miongoni mwa wadhanaishi wasiokuwa na uhakika kwamba Mungu yupo.


   MAREJELEO
Njogu, K. na Chimerah, R. (1999): Ufundishaji wa fasihi, nadharia na mbinu, Jomo Kenyata Foundation Nairobi.
Kezilahabi, E. (2008): Kichwa Maji, Vide-Muwa Publishers.Nairobi.
Wafula, R.N. na Njogu, K. (2007): Nadharia za uhakiki wa fasihi, Sai Industries limited. Nairobi.
Wamitila, K.W. (2003): Kamusi ya fasihi Istilahi na nadharia. Focus Publications limited. Nairobi Kenya

No comments:

Post a Comment