Thursday, July 14, 2016

UFEMINISTI KATIKA TAMTHILIA YA NATALA-KITHAKA MBERIA



Tamthilia: Ni utungo wa drama ambao  ni aina mpya ya maandishi ya sanaa  za maonesho, ta mthilia  ni ule utungo ambao waweza  kuwa umeandikwa  au haukandikwa (Temu 2003:206)
Tamthilia: Ni utungo wa fasihi ambao umebuniwa kwa kiasi kikubwa kwa lugha ya mazungumzo yenye kuzua na kuendeleza matukio ya hadithi ya utungo huo.
Hivyo basi tamthilia ni utanzu wa fasihi ulio andikwa kwa ajili ya kuigizwa jukwaani na huwa na  wahusika waliobeba ujmbe fulani.
Wahusika - ni viumbe wa hadithi wanaotokana na mawazo ya mwandishi au msimulizi, na wanaumbwa ili kuwasilisha ujumbe wa mwandishi au msimulizi (Njogu  na Chimera 1999: 45)
Wahusika - ni watu,ama viumbe waliokusudiwa wawakilishe dhana, mawazo au tabia za watu  katika kaz ya fasihi
Hivyo basi wahusika ni viumbe hai na visivyo hai  vinavyotumiwa na msanii katika kazi ya fasihi ili kuwasilisha ujumbe lengwa.
Nadharia: ni istilahi ya kijumla inayomaanisha miongozo inayomuelekeza msomaji wa kazi ya fasihi  kufahamu kazi ya fasihi katika vipengele vyake vyote (Njogu na Wafula 2013:2)
Nadharia- fikra, mawazo, dhana, maoni  maelezo (Mohamed na Said 2008:168).
Hivyo basi, Nadharia ni mwongozo au mawazo yanayomwongoza mtu kutenda jambo fulani.
Ufeministi (nadharia ya mtazamo kike). Hii ni nadharia inayokinzana na mikabala ya kiumeni  inayoonekana kupendelea  wanaume na kuwanyanyasa wanawake. (Njogu na Chimera, 1999:18).
Ufeministi hii ni nadharia inayoangalia na kujaribu kutatua matatizo yanayowakabili wanawake katika jamii inayotawaliwa na wanaume. (Wafula na Njogu, 2013:90)
Hivyo basi, ufeministi ni nadharia inayolenga kupigania haki za wanawake na kuweka wazi matatizo yanayowakumba au kuwakabili wanawake kutokana na minyonyoro inayotokana na mfumo dume na kupendekeza njia za kutatua matatizo hayo.
Nadharia hii ni jibu la mikabala ya awali na imeshika kasi zaidi mnamo miaka ya 80 na 90. Nadharia hii ina mielekeo mingi kutegemea itikadi na falsafa ya mhakiki.
·         Mielekeo mikali inayotoka Marekani inayochukuliwa kwamba “mwanaume ni adui wa mwanamke na kamwe mwanaume hawezi kushiriki katika ukombozi wa mwanamke”
·         Mwelekeo huu unachukulia kwamba tofauti za kimaumbile baina ya mwanamke na mwanaume si muhimu zinafananishwapo na mshabaha wao
·         Inasisitiza nafasi ya uchumi na uundaji wa matabaka katika uhusiano baina ya mwanamke na mwanaume yaani mwelekeo huu unafungamanisha ukombozi wa kiuchumi na ukombozi wa mwanamke.
Kwa mujibu wa Njogu na Chimera mihimili ya ufeministi ni kama ifuatavyo:
-        Inatumia fasihi kama jukwaa kuelezea kwa uyakinifu hali aliyonayo mwanamke katika jamii.
-        Nadharia hii inanuia kusawazisha wanadamu kwa upande wa utamaduni na uana.
-        Mtazamo huu vilevile unajaribu kuhamasisha utungaji wa kazi za sanaa zenye wahusika wa kike wanaoweza kuigwa.
-        Inakuza na kuendeleza hisia za umoja wa wanawake kama kundi linalodhulumiwa.
-        Nadharia hii inanuia kuzindua mwamko kwa upande wa mwanamke jinsi wanavyojiona na uhusiano wao na watu wengine.
-        Lengo muhimu la nadharia hii ni kuvumbua na kuziweka wazi kazi za kifasihi zilizotungwa na wanawake na ambazo zimepuuzwa kwa sababu ya utamaduni unaopendelea wanaume.
Kwa kuzingatia mtazamo kike mhusika Natala katika tamthiliya ya “Natala” ya Kithaka Mberia amesawiriwa kama ifuatavyo:
1.      Kutumia fasihi kama jukwaa kuelezea kwa uyakinifu hali aliyonayo mwanamke katika jamii. Mwanamke ameonekana kama mtu anayekumbana na matatizo mengi kwenye jamii. Hivyo wasanii hutumia fasihi kama sehemu muhimu katika kuelezea hali na matatizo aliyonayo mwanamke kwenye jamii.   mfano: katika kitabu hiki, Natala ameonekana  kama mwanamke jasiri, mhusika Natala alikuwa anaonewa kwa kutaka kunyang’anywa  mali yake na shemeji yake aitwaye Wakene, kutokana na ujasiri Natala aliweza kutetea mali yake katika uk.55:
Wakene : uondoe huo mkono!
Natala    : kilete cheti!
Wakene  : nitakutwanga!
Natala    : niguse uone! Tia mkono motoni.
Natala alikumbana na matatizo katika ndoa yake jambo ambalo limewakumba wanawake wengi katika jamii yetu ya sasa hasa pale ambapo wenza wao wanapokuwa mbali nao.
2.      Kusawazisha wanadamu kwa upande wa utamaduni na uana. Inapigania jamii mpya yenye misingi katika amali za binadamu. Baadhi ya amali ni zile za kike na za kijadi na ambazo zinadharaulwa katika jamii ya sasa mfano katika kitabu cha Natala uk 52 hati ya nyumba aliyoachiwa Natala ilileta mtafaruku mkubwa .Wakene anasema,
“Kaka yangu aliacha shamba na nyumba mali hii haina budi kubakia kwenye familia yetu na kwa sababu wewe mwenyewe umeamua kujitenga na familia yetu  hauwezi kuendelea kuitumia mali hiyo”
Pia Natala alifukuzwa lakini watoto wanabaki. Kwa hiyo basi mwanamke hana sauti hata kwa watoto wake jambo ambalo lipo katika jamii zetu nyingi za kiafrika.
3.      Mtazamo huu vilevile unajaribu kuhamasisha utungaji wa kazi za sanaa zenye wahusika wa kike wanaoweza kuigwa, wanawake ambao hawategemei wanaume ili wajitambulishe. Mfano katika tamthiliya yetu ya Natala.
Natala alisikilizwa pale alipokataa kuwa wasione mwili wa marehemu mume wake.
Natala alionyesha msimamo alipokataa kutoa rushwa ya ngono kwa mfanyakazi wa chumba cha maiti aitwaye Bala.
Natala alikataa kutoa rushwa kwa chief kwa ajili ya kutoa kibali cha kumzika mume wake.
Natala aliweza kuwalea watoto wake vizuri pamoja na kwamba alikuwa peke yake.
Natala alikataa kurithiwa na shemeji yake (Wakene).
Natala alionekana kama mwanamke mwenye busara. Hivyo basi hata katika jamii zetu wapo wanawake wanaoweza kujisimamia na kujiendesha katika shughuli zao bila kutegemea nguvu ya mwanaume. 
4.      Kukuza na kuendeleza hisia za umoja wa wanawake kama kundi linalodhulumiwa.
 Mfano katika tamthilia ya  Natala tunamuona mhusika Gane akimtia moyo Natala kwa kumuunga mkono katika harakati  za kutetea haki zake  uk 24 Gane anasema
Gane: Usivunjike moyo Natala mapenzi yako imara moyo wako wa kazi na nidhamu yako  thabiti   ni  baraka kubwa.
Baraka hizi zitakuwa jahazi la kuwafikisha watoto wako waendako, naamini hawataachwa nyuma na rika lao.
Natala: Ahsante kwa maneno yako ya kutia moyo. Pia tunawaona wahusika Natala na Gane  ni wanawake wanaopambana  ili kuondoa mila na desturi potofu zilizopitwa na wakati,  dhana hii imejitokeza pale Natala alipokataliwa kupewa   mwili wa marehemu mume  wake na alipotaka kunyanganywa hati ya shamba.
Hivyo basi hata  katika  jamii za sasa wapo wanawake wanaoshirikiana katika kuondoa mila na desturi  potofu   zilizo pitwa na wakati   zinazowakandamiza wanawake.
5.      Inanuia kuzindua mwamko kwa upande wa wanawake jinsi wanavyojiona, na uhusiano wao na watu wengine.
Mfano katika tamthilia ya Natala mwandishi amemtumia Natala kama mwanamke ambae ameweza kupambana na matatizo yanayo mkabili au kumkumba mwanamke katika jamii uk 22 tunaona pale Natala alipokataa kutoa rushwa ya ngono kwa Bala.
Bala    :  (kwa mshangao) lakini unasema umenielewa
Natala  : nakuelewa nini! Mimi sio mlango wa jengo la umma kuguswa na kila mtu
Bala    : (anajiweka tayari kumrukia Natala kazi bure! Moto  utazimwa leo utajua mimi ni mwanaume halisi).
Hivyo basi, mhusika Natala ameonekana kuzindua wanawake wengi kukataa rushwa ya ngono na vitendo vingine vya udhalilishaji vinavyowakabili wanawake wengi katika jamii, tunaona kwamba wanawake wengi wanadhalilishwa kwa kuwataka watoe rushwa ya ngono pale wanapokua wanatafuta kazi waajiri wengi huwataka wafanye hivyo.
6.      Kushirikisha wanaume katika harakati za kumtetea na kumkomboa mwanamke. Mfano katika tamthilia ya Natala mwandishi amemtumia mhusika Bala kama mwanaume anayeshirikiana na Natala kupambana na Wakene, kipindi Wakene anamnyang’anya Natala hati miliki ya shamba na pesa uk 56, (Bado akijaribu kuwatenganisha) Haondoki hapa na cheti.
Wakene : (kwa Bala) Niachilie wewe punda! Tangu kakaangu aage dunia umekuwa ukimmezea mate huyu mwanamke. Unafikiri hatujui kwanini ulishughulika sana kwenye mazishi?
Bala      : Usiropokwe na maneno, Wakene!
Wakene  : (Akimpiga Bala teke) usiniletee ubaladhuli!
Hivyo basi tunaona kwamba wapo wanaume ambao wamekuwa mstari wa mbele kuwatetea wanawake ili wasiendelee kunyanyaswa kwa vitendo viovu au mfumo dume.
7.      Kutumia wahusika wanawake katika kazi za fasihi. Katika tamthiliya hii mwandishi amejaribu kuwatumia wanawake kama wahusika ili kuwakilisha kundi kubwa la wanawake katika  jamii kwa lengo kuu la kuamsha hisia, mawazo,uelewa juu ya mambo mbali mbali yanayowakumba wanawake . mfano mwandishi alimtumia Natala, Tila, alika Gane.
Pamoja na kwamba nadharia hii ya ufeministi inajaribu kuyaweka wazi matatizo anayokumbana nayo mwanamke katika jamii kutokana na minyororo ya mfumo dume ambayo matatizo mengi ya mwanamke yanasababishwa na mwanaume au wanaume kama chanzo cha migogoro na matatizo kwa wanawake katika jamii pia wapo wanawake  ambao wananyanyasana   wao kwa wao mfano, Mama Lime uk 37.
Mama Lime   : Wakene yuko tayari kushirikiana na wewe
Natala             : Katika malezi ya watoto?
Mama Lime    : Maisha kwa ujumla, kukiwemo malezi ya watoto
Natala            : Unamaanisha nini maisha kwa ujumla?
 Mama Lime  : Wazee wamezungumza naye tayari yuko tayari kuziba pengo muhimu ambalo limeachwa na marehemu mumeo.
Natala               : Unamaanisha kuwa?
Mama Lime      : Kukuoa, tayari kuna misingi imara.
Hivyo basi, mwandish kwa kumtumia mhusika Mama Lime tunaona kwamba matatizo mengine ya wanawake yanatokana na wanawake wenzao yaani wananyanyasana wao kwa wao.

MAREJELEO
Mazrui, A.M. na  Syambo, B.K (1992). Uchambuzi na Fasihi.Nairobi: East Africa Educational publishers.Ltd 
Mberia,K, (1997).  Natala. Nairobi
Said, A.S.M (2008) Kamusi ya Visawe. Nairobi: East Africa Publishers.
Senkoro, F (2011) Fasihi. Dar es Salaam: KAUTU United Publishers
Temu, C.W (2003). Fasihi Nakala za Semina za Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili III. Dar es Salaam.
Wafula, R na Njogu, K (2007), Nadharia ya Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation Publishers

No comments:

Post a Comment